Mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha Dira TV na Kampuni ya Msama Promotions Limited, Ndg. Alex Msama, ametuma salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, na marafiki kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi, Ndg. Boniface Kikumbi, maarufu kama King Kikii, kilichotokea mapema leo, tarehe 15 Novemba 2024.
Akizungumza kwa masikitiko, Msama amesema: “Nimesikitishwa sana na kifo cha ndugu yangu kipenzi Boniface Kikumbi ‘King Kikii.’ Nimefahamiana naye kwa zaidi ya miaka 30 na tulifanya kazi pamoja kwa miaka 25. King Kikii alikuwa si tu mwanamuziki wa kipekee, bali pia rafiki wa karibu na mtu wa watu. Ninatoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, wasanii, na wapenzi wote wa muziki nchini kufuatia msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Aamin.”
Mchango wa King Kikii katika Muziki wa Tanzania huyu alikuwa mmoja wa wanamuziki mashuhuri wa muziki wa dansi nchini Tanzania.
Alijulikana kwa sauti yake ya kipekee, uandishi wa nyimbo zenye ujumbe wa kina, na umahiri wake wa kupiga gitaa. Alikuwa sehemu ya bendi maarufu kama Western Jazz na baadaye akaunda bendi yake mwenyewe inayojulikana kama King Kikii Orchestra.
Kupitia nyimbo zake kama “Safari ya Mombasa” na “Mpenzi Sikilizaa”, King Kikii aliwavutia maelfu ya mashabiki wa dansi kwa miongo kadhaa.
Muziki wake ulichangia kuimarisha hadhi ya muziki wa dansi nchini, huku akihamasisha kizazi kipya cha wanamuziki kuendeleza urithi huo.
King Kikii alitambuliwa kama msanii wa kipekee aliyechanganya ustadi wa muziki wa kitamaduni wa Tanzania na ladha ya kimataifa, na kujenga umaarufu wake hadi nje ya mipaka ya nchi.
Kazi yake itaendelea kuishi kupitia nyimbo zake na urithi aliouacha kwa tasnia ya muziki wa dansi.
Familia ya muziki wa dansi na Tanzania kwa ujumla imepoteza nguzo muhimu. Tunatoa pole kwa wote walioguswa na msiba huu. Roho ya marehemu ipumzike kwa amani.