Afisa Muelimishaji kutoka TAKUKURU – Ilala, Bi. Marcella Salu, amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa hayapaswi kuachwa mikononi mwa serikali au TAKUKURU pekee, bali ni jukumu la kila mwanajamii kushiriki kikamilifu.
Akizungumza katika mafunzo kwa watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Bi. Salu alisema kuwa TAKUKURU inafanya kazi kama nahodha katika vita hivi, lakini inahitaji ushirikiano wa jamii kwa ujumla, ikiwemo watumishi wa MNH na viongozi wao, ili kufanikisha mapambano haya, hasa kwenye idara zinazohusika na manunuzi.
“TAKUKURU ni kama nahodha anayeongoza, lakini nyuma yetu ipo jamii ikiwa ni pamoja na watumishi wa MNH na viongozi kwa ujumla wake ili kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa hasa katika idara za manunuzi,” alisema Bi. Salu.
Kwa upande wake, Afisa Muelimishaji mwingine kutoka TAKUKURU – Ilala, Bi. Nerry Mwakyusa, amewataka watumishi wa umma kuzingatia sheria na kanuni zote zilizowekwa katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutoa huduma bora na kwa haki kwa jamii. Alisisitiza kuwa ni muhimu kuwepo na ukaguzi wa ndani katika taasisi zote, ukihusisha mapitio ya kazi zinazofanyika na kutoa maoni yatakayosaidia kugundua viashiria vya rushwa mapema, ili kuzuia matatizo kabla hayajatokea.
“Ili kukabiliana na kupambana na rushwa, ni muhimu watumishi kuwa wawazi katika uwajibikaji kwa kuandaa nyaraka zote za utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, pamoja na kutotegemea mishahara pekee, bali pia kubuni miradi binafsi ya kujiongezea kipato ili kuepuka rushwa,” aliongeza Bi. Mwakyusa.
Mafunzo haya yalitolewa tarehe 1 Oktoba 2024, yakiwa ni sehemu ya juhudi za TAKUKURU kutoa elimu kuhusu mbinu bora za kudhibiti rushwa kwenye sekta mbalimbali.