Na WAF – Dar Es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu akiwa ameambtana na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu wametembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar Es Salaam ili kuona utayari wa nchi katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg na Mpox.
Akiwa katika ziara hiyo leo Oktoba 1, 2024 Dkt. Jingu amesema kinachofanyika katika uwanja huo ni kuandaa maeneo kwa ajili ya ukaguzi na vipimo kwa wageni mbalimbali wa ndani na nje wanaoingia nchini ili waweze kukaguliwa hali zao za kiafya.
“Tunapokea Wageni kutoka sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi, hivyo endapo akipatikana Mgonjwa atahifadhiwa na Sampuli zake zitachukuliwa kwa ajili ya kupelekwa Maabara ya Taifa kufanyiwa vipimo, hivyo nitoe rai kwa Wananchi wote tushirikiane lakini kubwa zaidi tuzingatie Ushauri wa Wataalam dhidi ya tahadhari zinazo tolewa”. Amesema
Dkt. John Jingu.
Aidha, Dkt. Jingu amesema ugonjwa wa Marburg ni hatari na ukimpata mtu humsababishia wakati mwingine kifo kwani mwaka 2023 ulipatikana mgonjwa Mkoani Kagera lakini ukadhibitiwa, hivyo nchi lazima ichukue tahadhari ya ugonjwa usiingie nchini ikiwemo kuhakikisha Mipaka inakuwa salama muda wote ikiwepo viwanja vya ndege.
Akisisitiza umuhimu wa elimu Kuhusu ugonjwa wa Marbug Dkt. Jingu amesema ni pamoja na kutoa taarifa kwa wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwemo njia ya vipeperushi katika maeneo mbalimbali katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere, runinga pia zinatumika kutoa ujumbe juu ya jinsi unavyoambukiza, dalili pamoja na namna ya kujikinga ili kusaidia wageni wanaoingia kuhakikisha wanajikinga.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikal Prof. Tumaini Nagu akizungumzia dalili za ugonjwa wa Maburg kuwa ni pamoja na homa, uchovu, kuharisha, kutoka damu sehemu mbalimbali za mwili hivyo ametaka wananchi kutoa taarifa haraka ikiwa ataona mtu ana dalili za hivyo ili awahishwe kupata matibabu.