Na Sophia Kingimali.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema matukio ya utekaji, Kulawiti, Kunyanyasa, Ubakaji, Utekaji na Mauaji yanayoendelea nchini yanatia aibu na doa kwenye nchi, hivyo amewataka viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwajibika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10,2024 jijini Dar es salaam Mkurugenzi huyo amesema kutokana na sakata hili ingepaswa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Yusuph Hamad Masauni, pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wanapaswa kuwajibika.
“Hizi tabia mbaya zilizozuka katika taifa letu, za kuteka, kuuwa, kunyanyasa na kulawiti watanzania wenzetu. Tunaye Rais mmoja na sio wawili au watatu tuliyemkabidhi katiba yetu, ili aitumie kuongoza na kulinda taifa letu na kuhakikisha usalama wa watu wote wakiwemo wageni na mali zetu kwa mujibu wa katiba,” amesema na kuongeza kuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani na wakuu wa vyombo vya ulinzi wasituambie hawajui, hawa wanafuata na Rais wakati wote, sifatani na rais mimi, lazima wajue, wanapaswa kuwajibika kwani hii ni aibu kwa Rais na taifa,” amesema.
Amesema tatizo la mauji, utekaji, ulawiti, utesaji halijaanza leo, hata kipindi cha Rais John Magufuli, Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa, Alhaji Hassan Mwinyi na Mwalimu Julius Nyerere yalikuwepo, ila watu waliwajibika.
Amesema kipindi cha Hayati Nyerere aliweza kuondoa uongozi wote wa jeshi la polisi, lakini pia Hayati Mwinyi alijiuzulu, Abdallah Natepe alijiuzulu kwa makasa ambayo hawakufanya, hivyo ni wakati muafaka kwa viongozi hao kujiuzulu ili kumpa nafasi Rais Samia ya kuteua wengine.
“Jambo la kuwajibika naona kama vile linafifia, huwezi kuona watu wanakufa kila mahali, wanaelea baharini na kwingine, halafu wewe Waziri unasema Rais ameagiza, unangoja akuagize bila wewe kuwajibika,” amesema.
Butiku amesema Tanzania sio taifa la wauji au wahuni na kwamba watu wake wanaishi kwa mujibu wa katiba, hivyo kila mtu anatakiwa kuzingatia hilo na hakuna nafasi ya mtu yoyote kumfanya mwingine aishi nje ya misingi ya ustaarabu.
“Tusiseme hatuwajui wahalifu hao, tunawajua, wanaishi miongoni mwetu, katika kaya zetu, wapo ndani ya vyombo vyetu vya dola, wapo makanisani na misikitini, tunawajua, lazima serikali yetu iwajue, hivyo MNF inaomba wananchi wamsaidie Rais kupata taarifa sahihi kuhusu wabaya wetu hao, ili aweze kuchukua hatua stahiki.
Rais anavyo vyombo vya dola ambavyo vinauwezo wa kuchunguza na kubaini matukio hayo kwani miaka 60 ya uhuru kuwatambua wahusika ni rahisi,” amesema.
Butiku amesema viongozi wa vyombo vya dola wasithubutu kusema hawajui wahusika, kwani wanajua na wasiseme wanamuogopa Rias na kwamba kusema hivyo ni kumsingizia.
Aidha, akijibu swali kuhusu hitaji la kuomba wachunguzi kutoka nje, kutokana na wananchi kukosa imani na vyombo vya dola nchini, amesema iwapo itaonekana ni muhimu kufanya hivyo wanaweza kufanya hivyo, huku akiweka bayana kuwa kwa uzoefu wake anaona vyombo vya ndani vina uwezo, kwani watendaji wa uhalifu huo wapo ndani yetu.
Aidha Mzee Butiku amewataka wananchi kuacha kunyoosheana vidole, huku akiwataka vijana waache uoga wa kudai haki na kwamba Baba wa Taifa aliacha usia kuwa watanzania wasiogope kwani wakiogopa watakuja kutawaliwa na wahuni, wezi na wauaji.
Mkurugenzi huyo pia amevitaka vyombo vya habari kusimamia misingi na taaluma ya habari, kwani wapo baadhi ya waandishi na vyombo ambavyo vinatumika vibaya jambo ambalo linaondoa dhana nzima ya uzalendo.
“Katika mambo ya aibu kwenye nchi yetu, hili la mauji ni la iabu, hivyo nadhani mamlaka zinaweza kutafakari kwa kina ili kupata muafaka kwenye hili”,Amesema.