Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito kuwa matamasha yanayoandaliwa yatumike katika kukumbushana agenda za kitaifa ikiwemo ya mazingira.
Ametoa wito huo baada ya kushiriki uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi katika Uwanja wa Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja leo Agosti 18, 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Mhe. Khamis amesema ni jambo la muhimu kutumia matamasha pia katika kufanya uzinduzi wa miradi ya huduma za kijamii ikiwemo ya elimu na afya badala ya wananchi kukutana na kusherehekea na kutawanyika.
Aidha, ametoa pongezi kwa waandaji na washiriki wa Tamasha la Kizimkazi 2024 akisema kuwa limeendana na agenda mbalimbali muhimu zinazogusa maisha ya binadamu ikiwemo ya mazingira.
Naibu Waziri Khamis amesma kuwa tamasha hilo limeenda sanjari na kongamano kubwa la nishati safi ya kupikia ambalo lilitumika katika utoaji wa elimu ya namna ya kutunza vyanzo vya maji.
“Kama mnavyofahamu Mkoa huu wa Kusini ni ukanda wa bahari hasa maeneo ya Paje, Makunduchi, Jambiani na Kizimkazi hivyo hatuna budi kuipa kipaumbele elimu ya namna ya kutunza vyanzo vya maji, namna ya kufanya
uvuvi usioathiri viumbe vya baharini vikiwemo samaki, matumbawe (makazi ya samaki) na maji kwa ujumla,” amesisitiza.
Halikadhalika, Naibu Waziri Khamis amesema wakati Serikali inachagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia, Tamasha la Kizimkazi limesukuma agenda hiyo ambapo elimu ya kutumia nishati hiyo imetolewa hivyo kusaidia katika
kuwabadilisha wananchi kuachana na vitendo vya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Amesema kwakuwa Mkoa wa Kusini unapakana na bahari, katika tamasha hilo agenda ya uchumi wa buluu imechukua nafasi yake kwani ni moja ya hatua za kukuza uchumi hivyo, wananchi wamehimizwa kusafisha fukwe ili ziwe safi na kuendelea kuvutia watalii wanaozuru Zanzibar.
Akizungumzia zaidi kuhusu tamasha hilo, Naibu Waziri Khamis amesema tamasha la mwaka huu limefanya vizuri na kuwa na mvuto zaidi kwani limeshirikisha wadau mbalimbali hivyo kuweza kukuza uchumi kutokana na
jamii ya wajasiriamali kuwa na ushiriki mkubwa.
Amesema tamasha hilo limekwenda sanjari na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itakuwa na tija kubwa wananchi ikiwemo skuli kubwa za kisasa, vituo vya afya, vituo vya polisi, barabara na maji.
Naibu Waziri Khamis ameongeza kuwa ratiba ya mwaka huu imekwenda mbali
zaidi kwa kufanyika uzinduzi wa kiwanja kikubwa cha kisasa cha michezo na
vituo vya ujasiriamali Kizimkazi.