Na John Bukuku Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan anatarajia kuhudhuria Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 17 Agosti 2024 mjini Harare, Zimbabwe.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais Mhe. Dkt. Samia anaondoka nchini leo Agosti 15, 2024.
Mkutano huo wa 44 wa SADC utatanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Troika chini ya Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais Haikande Hichilema wa Zambia anayekabidhi uenyekiti huo itakutana kesho Agosti 16 kumteua Rais Dkt. Samia kuwa Mwenyekiti mpya wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ on Politics, Defence and Security Cooperation)
Rais Dkt. Samia atashika uenyekiti huo kwa kipindi cha mwaka mmoja na atapokea kutoka kwa Rais wa Zambia
Mhe. Hakainde Hichilema aliyemaliza kipindi chake cha uenyekiti cha mwaka mmoja.
Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC.
Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025.