Utamaduni ni mfumo wa maisha ya kila siku katika jamii ya watu fulani, kila jamii huaamini iko sahihi katika mifumo yao ya maisha dhidi ya tamaduni za jamii nyengine.
Mifumo hiyo inaweza kuwa katika vyakula, namna ya kuendesha baadhi ya shughuli kama arusi, misiba, michezo na burudani na hata mitindo ya mavazi.
Kuna baadhi ya jamii zinasimamia na kuendeleza tamaduni zao licha ya kuwa zinaonekana kuwa kikwazo kwa baadhi ya wanajamii hao kwani baadhi ya tamaduni hizo huwakandamiza, kuwabana na kuwanyima fursa za mambo mbalimbali ya kijamii , kisiasa, maendeleo na hata kiuchumi.
Utamaduni wa mavazi ya stara na shurti ya kushiriki michezo isiyo na mchanganyiko wa jinsia mbili kunafanya ushiriki wa wanawake kuwa mgumu zaidi hasa wacha Mungu.
Uzowefu unaonesha kuwa kukosekana kwa mavazi hayo kwa jamii ya watu fulani kuchangia wanawake kutoshiriki katika michezo kikamilifu.
Aidha kulihusisha suala la michezo , kwa wanawake na uhuni au kukosa maadili kunapelekea wanawake wengi kutokutaka kushiriki katika michezo kwa kuogopa jamii kuwatizama kwa mtazamo hasi .
Licha ya kuwa michezo kama Mpira wa Miguu, Mpira wa Magongo, Kriketi, Mpira wa Meza, Mpira wa Vinyoya, Riadha, Mbio za Punda na Farasi, Mchezo wa Ngombe, Karata na Bao pamoja na michezo mengine,ilianza tangu miaka ya 1875 visiwani Zanzibar ,lakini bado michezo hiyo haikuwashirikisha wanawake ipasavyo, kutokana na jamii hiyo kuamini mwanamke ni kwaajili ya majukumu ya nyumbani na muhusika wamichezo ni mwanamme pekee.
Baadhi ya wanawake na wasichana mara nyingi hushiriki katika michezo wakiwa mashuleni na mara wamalizapo masamo yao ,michezo hubaki kuwa kitendawili kisichotegulika.
Wakati Zanzibar inaaza michezo miaka ya 78 ilikua ni sehemu ya kujiburudisha tu licha ya kuwa ilichezwa kwa ustadi mkubwa na kuvutia watazamaji, sasa michezo ni biashara na fursa na kila mmoja anahitaji kuifikia fursa hiyo.
Makala hii itaangazia kwa kiasi gani tamaduni, mila ,silka ,desturi na maadili kwa baadhi ya jamii zinakwamisha wanawake na wasichana kushiriki katika michezoipasavyo.
MITAZAMO YA JAMII YENYEWE
Mohammed Ramadhan Khamis mkaazi wa Maungani wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa Makala hii alisema kuwa ushiriki wa wanawake katika michezo si jambo zuri na si katika maadili ya jamii ya wazanzibari.
Alieleza kuwa michezo ni harakati za kushughulisha viungo na vile maumbile ya mwanamke yalivyoumbwa kunaweza kutokea ushawishi utakaochochea vitendo vya udhalilishaji. “ile mitetemotemeko ya maungo ya watoto wa kike inaweza kushajihisha utovu wa nidhamu na kupelekea mporomoko wa maadili”alisema bwana huyo
Bwana Mohammed anaamini kuwa ili kulinda maadili na tamaduni za msichana wa kizanzibari, ni kutokumshirikisha katika michezo hasa ya kimagharibi.
Alitumia fursa hiyo kuwashauri viongozi wa nchi kuweka mikakati ya kuelimishana juu ya athari zitakazotokezea ambapo wasichana watashiriki katika michezo bila kuzingatia mila na desturi zao.
“tusilazimishe mwanamke kufanya harakati ambazo ni kinyume na tamaduni mila na desturi zetu na kuondoa heshima zao”Alimalizia
Makala hii ilizungumza na bi Abeda Rashid Juma mkaazi wa Mwambale Mkoa wa kaskazini Unguja ambapo alieleza kuwa kumshirikisha msichana wa katika michezo ya kimagharibi i njia moja ya kuupoteza utamaduni wa Mzanzibari.
“Mavazi ya michezo inayohamasishwa sasa si katika mila na desturi zetu kwani yanaruhusu umbile lote la mtoto wakike kuonekana.” Alileleza bi Abeda
Alisema jamii yao hairuhusu mwanamke kushiriki kwenye michezo hasa ya kimagharibi ili kuendelea kulinda milka ,silka na tamaduni zao.
“sio kama watoto wetu wa kike hawachezi , watacheza dama, nage , udako na sio mpira wa miguu hayo ni mambo ya wazungu tusiwe tunaiga tu hata mambo ambayo yanapoteza utamaduni wetu”
Bi Masha Abdalla Sleiman mkaazi wa Jang’ombe wakati anazungumza na makala hii alisema kumshirikisha mwanamke na msichana katika michezo kunawezekana pale ambapo wadau wa michezo wataangalia mchezo gani maeneo gani na kwa namna gani ili kulinda utamaduni, nidhamu , na heshima ya mwanamke.
Alieleza kuwa ipo baadhi ya michezo ya kumshrikiha mtoto wa kike lakini michezo ya sasa kwa maadili ya mswahili wa kizanzibar sio busara kumshirikisha.
Alitolea mfano wanamichezo wa kike nchini Iran alisema wanawake hao walishiriki katika michezo ya kulenga shabaha tu kwa sababu haikukiuki kanuni ya mavazi ya tamaduni zao.
Mwisho alizishauri kampuni za vifaa vya michezo kubuni mavazi ya michezo yanayokubalika katika kila tamaduni ili mwanamke aweze kushiriki bila kuathiri utamaduni wa mavazi ya jamii yake.
Kwa upande wa Mkoa wa kusini makala hii ilizungumza na Nachiani Pandu mwenye (65) mkaazi wa Mzuri Makunduchi ambapo alisema,kucheza kwa mtoto wa kike si suala geni, ubaya ni kuwa tumeacha kucheza michezo ya asili inayolinda tamaduni zetu na kufuata umagharibi.
Alisema hali hiyo inapelekea watoto wa kike kukiuka maadili yao.
“Michezo yetu ya asili ndio michezo pekee inayofaaa kuchezwa na wanawake na sio mpira wa miguu na ile michezo ya kuruka na mpira ukiwa na nguo fupi zinazouwacha nusu ya mwili wa msichana kuwa nje.”alisema mama huyo
Alisema ipo haja kwa Serikali kufanya tafiti kujua michezo ipi wanawake wa Zanzibar watashiriki huku wakiendelea kulinda mila ,desturi heshima na maumbile ya mwanamke.
“Ikiwa tunataka kuwashirikisha wanawake katika michezo, tuirudie michezo yetu ya asili iliyokua ikichezwa kwa heshima na nidhamu na bado tunafurahia michezo hiyo, sio kuhamasisha wanawake kushiriki michezo bila kuangalia kwa kiasi gani inaathiri mila na desturi za jamii wanazozihamasisha” alisema mama huyo
AFISA UTAMADUNI
Mikidadi Mwadini Ali ni Afisa utamaduni idara ya utamaduni wakati akizungumza na makala hii alisema kuna umuhimu wa wanawake kushiriki katika michezo kwa maendeleo lakini ni lazima mila na desturi ziendelee kulindwa.
“hapo zamani wanawake walikua wanacheza michezo inayowahusu tu kama nage ,mdako ,hadimfundo na mara chache ndio walicheza michezo inayohusishwa kuwa ni ya wanaume kama karata na bao la kete.” Alisimulia afisa huyo
Aliendelea kwa kusema kuwa michezo yote hiyo haikuathiri maadili na tamaduni za mzanzibar kama ilivyo michezo ya sasa ambayo imeigwa kutoka tamaduni zisizo za kwetu.
Afisa utamaduni alishauri kuongezewa thamani michezo ya asili kwa kuwashindanisha na kuwapatia tuzo kama ni sehemu ya mafanikio na maendeleo kupitia michezo na hiyo itasaidia kuitrithisha kwa vizazi vijavyo na kuwa sehemu ya kukuza utalii kupitia michezo ya asili..
Alisema Mwanamke kucheza mpira wa miguu ni tamaduni za nchi za magharibi ambazo sasa Zanzibar tunajaribu kuziiga bila kujali kwa kiasi gani zitaathiri tamaduni zetu na kutangaza utamaduni wa nchi nyengine.
“tunapozungumzia utalii wa kimichezo sio michezo ya kimagharibi kwani watalii walishazowea kuiona michezo hiyo nchini kwao, kupitia michezo yetu ya asili watalii watavutika kuiangalia na kuwa sababu ya wazanzibar kunufaika kupitia michezo yao ya asili.”alisema afisa utamaduni
Alisema mtazamo wake ni kuwa jamii isiitumie fursa ya za michezo kama sababu ya kupoteza asili na tamaduni zeo ,ingawaje utamaduni unaweza kubadilika kutokana na wakati na mazingira, lakini jitihada zinahitajika kuhakikisha utamaduni hasa wa mavazi unabaki kuwa uleule kwa watoto wa kike wanaposhiriki michezo.
Mwisho afisa huyo aliwashauri wadau wa michezo kwa maendeleo kuangalia namna ya kulinda mila , tamaduni na desturi za wazanzibar kabla ya kuhamasisha wanawake kushiriki katika michezo.
IDARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WATOTO
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya jamii jinsia na watoto Siti Abas Ali wakati akizungumza na makala hii alisema sera ya michezo inaonesha wazi kuwa michezo ni haki kwa wote,kinachomshangaza ni kuona bado upande wa watoto wa kike ushiriki wao ni mdogo.
Alisema hiyo ni kutokana na tamaduni za baadhi ya jamii kutokumpa umuhimu msichana kushiriki katika michezo na kumhusisha na kazi za nyumbani tu.
Alisema bado kuna baadhi ya jamii zinaamini kuwa mwanamke kushiriki katika michezo ni kukaribisha vitendo vya kihuni jambo ambalo sio sahihi, na badala yake wanachotakiwa ni kutoa haki sawa kwa jinsia zote kupata nafasi za kushiriki katika michezo, huku jamii wakiwasimamia vyema wasichana kulinda madili na tamaduni zao.
Alifahamisha kuwa kuna umuhimu wa kumshirikisha msichana katika michezo kwani mbali na kujenga afya zao lakini pia wanapata uelewa wa mambo mbalimbali ikiwemo kujitambua, n ahata kujikinga na vitendo vya udhalilishaji .
Mkurugenzi siti aliwashauri wadau wa michezo kwa maendeleo kutoa elimu kwa viongozi wa dini,jamii zenye mtazamo hasi na waandishi habari juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika michezo.