Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na UtawalaBora, Mhe. Deus Sangu akizungumza leo na wananchi wa Kata ya Lusaka , Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawangamkoani Rukwa , ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Sehemu ya wananchi wa Kata ya Lusaka, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu mara baada ya kuwasili katika Kata ya Lusaka , ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Lusaka wakimlaki Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu mara baada ya kuwasili katika Ofisi za CCM Mkoa wa Rukwa, Ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha Lowe mara baada ya kufanya mkutano wa Hadhara uliofanyika, ikiwa ni ziarayake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu akizungumza na Katibu wake Bw. Juma Ijumaa wakati wa mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Kasulu, ikiwa ni ziarayake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
…………..
Na. Lusungu Helela
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kwela, Mhe. Deus Sangu amepiga marufuku Walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakiwemo wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 65, wenye ulemavu, akina mama wajawazito pamoja na watoto kufanya kazi za kujitolea huku akionya Watendaji watakaozembea kusimamia suala hilo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao
Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na Wananchi wa Kata ya Lusaka kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye vijiji vya Lowe, Lusaka, Kizumbi na Kamnyazya vilivyopo Jimbo la Kwela , Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa, Ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Amezitaja kazi hizo za kujitolea ambazo huratibiwa na TASAF kuwa ni ulimaji wa barabara pamoja na uchimbuaji wa mitalo ya barabara
Amesema kundi hilo lisisumbuliwe kufanya kazi hizo kwani sio sawa kutokana na hali zao.
Katika hatua nyingine Mhe. Sangu amezitaka Kaya zinazonufaika na Mpango wa TASAF kuhakikisha kama zina wanafunzi waliohitimu kidato cha sita na wanatarajia kujiunga Chuo Kikuu wawasilishe majina yao katika Ofisi za Halmashauri zao ili waweze kupata kipaumbele cha kupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu utakaowawezesha kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu kwani Bodi hiyo imeingia mkataba na TASAF
Amesema lengo la TASAF kuingia mkataba na Bodi ya Mikopo wa Elimu ya Juu ni kuhakikisha watoto wanaotoka katika Kaya maskini hawakosi mkopo ili kuhakikisha wanafaulu ili badae waweze kurudi kwa ajili ya kuzikomboa Kaya zao kwenye lindi la umaskini.
Amesema ni jambo lisilokubalika chini ya Uongozi makini wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona Mtoto aliyetoka kwenye kaya maskini kasoma na wazazi wake ni wanufaika wa TASAF lakini anakosa mkopo anapotaka kujiunga Chuo Kikuu
Kufuatia hatua hiyo Mhe.Sangu amewaagiza Waratibu wa TASAF wa Mikoa pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wana wasaidia watoto hao ili waweze kutimiza ndoto zao
Aidha, Mhe.Sangu amezitaka Kaya zenye watoto ambao ni Walengwa wa Mpango wa TASAF lakini Watoto hao hawajabahatika kujiunga kidato cha kwanza wachangamkie fursa ya ufadhili wa masomo unatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kujiunga VETA.