Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka wadau wa Sheria kuzingatia Weledi na Ubora katika kutekeleza majukumu yao kwenye maeneo yao ya kazi, Mwanasheria Mkuu ameeleza hayo wakati akifunga kikao kazi kilichowahusisha Wakurugenzi wa Divisheni, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Sheria kutoka Wizara, Taasisi na Halmashauri nchini.
Aidha, Mhe. Mwanasheria Mkuu aliwapongeza washiriki wote wa kikao hicho kwa kuhudhuria huku akiamini mada na mijadala iliyowasilishwa kwenye kikao hiki zitaenda kuwa chachu ya mafaniko kwenye majukumu yao ya kila siku.
“Niwapongeze kwa
kuhudhuria kikao hichi na niwashukuru watoa mada kwa kufanya mawasilisho, pia niwashukuru ninyi kwa usikivu wenu, maswali mliyouliza na mijadala mliyochangia naamini mkitoka hapa mtakwenda kuongeza kasi ya utendaji kazi kwenye maeneo yenu”. Alisema Mhe Mwanasheria Mkuu.
Katika hatua nyingine Mhe. Mwanasheria Mkuu amesisitiza juu ya suala la uanzishwaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria kwenye Mikoa na Wilaya, kwakuwa kamati hizo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi katika ngazi za Mikoa na Wilaya.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amemaliza hotuba yake fupi ya kufunga kikao hicho kwa kuwataka washiriki kufanya kazi kwa bidii huku akiwaahidi kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iko tayari kutoka ushirikiano kwa washiriki wakati wowote.