Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Suleiman Serera amekabidhi Bendera ya taifa, vifaa vya michezo na gharama za kujikimu kwa wachezaji wa timu ya Taifa inayokwenda Jijini Paris nchini Ufaransa kwenye michezo ya Olimpiki 2024 itakayotimua vumbi kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11, 2024.
Akizungumza wakati wa tukio hilo leo Jijini Dar es Salaam, Dkt. Serera amewataka wawakilishi hao wakiwemo wa timu ya kuogelea, riadha na Judo wakaipeperushe vyema Bendera ya Tanzania kwa kurudi na ushindi huku akisisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iko pamoja nao katika safari hiyo ya ushindi.
Aidha, ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lihakikishe linavisimamia vyama vya michezo kuandaa na kuwasilisha mipango yao ya maandalizi ya michezo ijayo ya Olimpiki itakayofanyika nchini Marekani mwaka 2028 .
“Mwaka huu tunawakilishwa na wachezaji saba lengo letu ni kuona mwaka 2028 tunapeleka idadi kubwa ya wachezaji na Serikali itaendelea kushirikiana na mashirikisho ya michezo ili kufanikisha malengo haya,” amesema Dkt Serera.