Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kutoka kwa Madaktari Bingwa kutoka Taassi ya moyo ya Jakaya Kikwete ambao wamepiga kambi ya siku 7 wilaya humo kwa ajili ya kutoa huduma za magonjwa ya moyo.
Na Mwandishi wetu, Namtumbo
……………..
Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) wamepiga kambi ya siku saba wilayani Namtumbo kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa wilaya ya Namtumbo.
Akizindua huduma hizo Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa alisema, zoezi la uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi litasaidia kuokoa maisha ya watu wengi ambao awali walishindwa kupata huduma hizo kutokana na gharama ya kufuata matibabu nje ya wilaya ya Namtumbo ikiwemo Hospitali ya Rufaa Songea,Peramiho na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kawawa,ameishukuru Serikali kupitia taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI),kwa kuleta Madaktari Bingwa watakaotoa huduma kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo,uzito mkubwa na presha.
Alisema,zoezi hilo litasaidia kuokoa maisha ya Watanzania hususai wakazi wa Namtumbo wanahitaji kupata huduma za uchunguzi lakini kutokana na changamoto mbalimbali hawakuweza kuzipata.
“taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete inarajia kuitumia Hospitali ya wilaya Namtumbo kama kituo kidogo cha uchunguzi wa Matibabu ya moyo ili kusaidia wananchi wenye hali ya chini mkoani Ruvuma kupata huduma karibu za matibabu”alisema Kawawa.
Aidha Kawawa,ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta zaidi ya Sh.bilioni 2.3 zilizosaidia kuboresha miundombinu ya Afya katika Hospitali ya wilaya Namtumbo.
Alisema,fedha hizo zimetumika kujenga jengo la huduma za meno, macho,jengo la mama ngojea na jengo la Mama,Baba na mtoto.
Hyera,uwekezaji wa miundombinu katika sekta ya afya wilayani humo umewezesha kutoa huduma kwa ubora zaidi hasa ikizingatiwa baadhi ya vijiji viko umbali wa zaidi ya kilometa 200 kutoka makao makuu ya wilaya Namtumbo mjini na vituo vya afya vilivyopo.
Pia alisema,wataalam hao watasaidia kuwapatia ujuzi zaidi wataalam waliopo wilaya humo hasa kwenye masuala la moyo na wananchi watapata huduma za magonjwa hayo bila kwenda mikoa mingine kufuta huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa kuwa zitapatikana katika Hospitali ya wilaya na vituo vya afya vilivyopo katika wilaya hiyo.
Kiongozi wa Timu ya Madaktari kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dkt Baraka Ndelwa alisema,zoezi hilo litafanyika kwa muda wa wiki moja na katika Hospitali ya wilaya,kituo cha afya Lusewa na kituo cha afya Mputa.
Alisema,katika zoezi hilo wanapima magonjwa ya moyo,kisukari na wananchi watapata elimu ya namna gani ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa na wale watakaobainika kuwa na shida kubwa watapewa rufaa ya kwenda Muhimbili.
Ametoa wito kwa wananchi wa Namtumbo, kutumia fursa hiyo kwenda kupata huduma ya uchunguzi wa magonjwa hayo ili kufahamu hali za afya zao.