Angela Msimbira MOROGORO
Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa ametoa rai kwa wakuu wa shule za msingi nchini kuimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji.
Pia kuongeza ubunifu katika utatuzi wa changamoto za ujifunzaji kwa wanafunzi ikiwemo matumizi ya zana na vifaa vilivyoboreshwa katika ufundishaji.
Dkt. Mtahabwa ametoa rai hiyo leo Julai 4,2024, mkoani Morogoro alipokuwa akifungua mafunzo ya siku 3 kuhusu miongozo mbalimbali kupitia Program ya Mboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).
Miongozo hiyo ni ya ujenzi, taratibu za manunuzi, usalama wa jamii na ufuatiliaji na tathimini na mfumo wa usimamizi wa fedha.
Dkt. Mtahabwa amewataka kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa maboresho ya ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi wa Darasa la Awali kwa kuwa ndio msingi wa wanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
Pia amewaagiza walimu hao kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa mpango wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) ili kuleta mapinduzi makubwa katika ufundishaji na ujifunzaji.
“Nanawaelekeza walimu wakuu kote nchini kwenda kuweka mazingira rafiki yatakayowavutia walimu wote kushiriki kikamilifu katika MEWAKA. Changamoto za utekelezaji zilizopo ndani ya uwezo wa shule mzitafutiwe ufumbuzi na muwe na ushirikiano na wadau wengine wakiwemo viongozi wenu wa Kata na almashauri,” amesisitiza Dkt. Mtahabwa.
Pia amewataka kuhakikisha wanaweka mifumo na mikakati ya kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa kuweka utaratibu na vilabu vya wanafunzi na kuwajengea uwezo wanafunzi kujitambua, kujieleza, na kujiamini.
“Shirikianeni na jamii kwa kuweka utaratibu wa kubaini na kushughulikia masuala ya ukatili, unyanyasaji na malalamiko yanayojitokeza ikiwemo kuyafikisha kwenye mamlaka husika kwa yale yaliyo juu ya uwezo wa shule kwa kuwa ulinzi na usalama wa mtoto ni kipaombele cha walimu” amesema Dkt.Mtahabwa