Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, akielezea umuhimu wa kuweka akiba kwa Wananchi wa Wilaya ya Sikonge, wakati wa semina iliyotolewa kwa wananchi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wilayani humo
Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella John, akieleza umuhimu wa kuwewekeza kwa Wananchi wa Wilaya ya Sikonge, wakati wa semina iliyotolewa kwa wananchi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wilayani humo.
Mkazi wa Kata ya Tutuo, Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Tabora, Bw. Daniel Kadete, akiuliza swali kuhusu kiwango cha riba kinachotambulika na Serikali kwa Timu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika wilayani humo kutoa elimu ya fedha.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Sikonge, wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo Watumishi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Tabora)
…………..
NA: JOSEPHINE MAJULA, WF, TABORA
Wajasiriamali wa Kata ya Tutuo, Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Tabora, wameiomba Serikali kuwapatia elimu ya ujasiriamali ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora, ambazo zitakidhi ushindani wa soko ili kujikwamua kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wajasiriamali Kata ya Tutuo, Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Tabora, Bi. Doroth Mgombela, alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika wilayani humo, kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi ili waweze kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya fedha kujikomboa kiuchumi.
“Tunaomba tupatiwe elimu ya ujasiriamali ili bidhaa zetu ziwe na mwonekano mzuri, ambao utamvutia mnunuzi lakini pia ziweze kukubalika katika soko la ndani na nje ya nchi ili kipato chetu kiweze kukua,” alisema Bi. Doroth Mgombela.
Aliongeza kuwa changamoto wanayokutana nayo katika shughuli ya ujasiriamali ni bidhaa kutokidhi mahitaji ya soko, lakini pia wanatumia njia za kienyeji kutengeneza bidhaa zao ambapo wanatumia muda mwingi kuzalisha bidhaa chache lakini pia kutokuwa na uhakika wa soko kutokana na bidhaa hizo kukosa ubora.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Tabora, Bi. Katoke Kisigiro, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo wanavikundi, wajasiriamali, watumishi, wanafunzi na wafugaji, aliahidi kuendelea kuwasimamia na kuhakikisha wanaitumia vizuri elimu ya fedha katika shughuli zao za kiuchumi na kujiongezea kipato kwa kujiwekea akiba, kufanya uwekezaji mbalimbali lakini pia kukopa mahali sahihi.
Naye Afisa Mtendaji Kata ya Tutuo Wilaya ya Sikonge, Bw. Alexander Mushongi, aliishukuru Serikali kwa kuweza kuwafikia na kuwapa elimu muhimu ya fedha itakayokuwa mkombozi kwa wananchi na anaamini kupitia elimu waliyoipata wananchi hao watafanya uwekezaji kwenye shughuli ambazo zitawaingizia kipato na kuwainua kiuchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, alisema kuwa katika maeneo mbalimbali waliyofika kutoa elimu kwa wananchi, mwitikio ulikuwa mkubwa na wananchi wameonesha utayari wa kubadilika na kuahidi kutumia taasisi rasmi kukopa, kuwekeza na kuanza kujiwekea akiba.
“Tunawashukuru na kuwapongeza Wananchi wa Mkoa wa Tabora kwa kujitokeza maeneo mbalimbali kupata elimu ya fedha maana bila wao kufika zoezi letu lisingefanikiwa, kwa upande wa maoni na ushauri tunaahidi kuyazingatia awamu ijayo”, Bi. Limi Bulugu.
Alisema hadi sasa mikoa nane imefikiwa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha na kupatiwa elimu ya fedha ikiwemo mkoa wa Kagera, Manyara, Singida, Kigoma, Rukwa, Simiyu, Shinyanga na Tabora.