Mbunge wa Bunge la EALA nchini Tanzania,J ames Ole Millya akizungumza Bungeni 
Mbunge wa Bunge la EALA  kutoka Tanzania  DkT. Abdullah Makame akielezea kuhusiana na bajeti hiyo.
Spika wa Bunge la EALA, Joseph Ntakirutimana akizungumza bungeni hapo na wabunge wa EALA. 
…………
Happy Lazaro,Arusha .
Wabunge wa bunge la Afrika Mshariki (EALA) wameshauri Viongozi wakuu wa nchi  wanachama wa jumuiya ya Afrika kusaidia kuzungumza na nchi  ambazo bado zinasuasua  katika utoaji wa michango ili ziweze kuchangia kama ambavyo nchi zingine zinafanya.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha katika vikao vya bunge hilo vinavyoendelea katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki,Mbunge wa EALA nchini Tanzania,James Ole Millya amesema kuwa, nchi kama Tanzania,Kenya na Uganda wanachangia kwa asilimia mia moja ila kuna nchi ambazo michango yake inasuasua hali ambayo inachangia kukwama kwa shughuli za maendeleo katika maeneo hayo.
Millya amesema kuwa, ni vizuri wakuu wa nchi wa jumuiya hizo wakakaa pamoja na kuweza kuzisukuma  nchi hizo ili ziweze kutoa michango  hiyo kwa wakati na kuharakisha maendeleo  katika nchi hizo .
“Leo bajeti imesomwa hapa bungeni ambayo ni Dola milioni  112.9  na bajeti hii inatia matumaini ila hofu kubwa Sisi kama wabunge tunaonea  huruma nchi zinazochanga kwa asilimia mia moja kama Tanzania,Kenya na Uganda wakati kuna nchi hazichangii kabisa na tumewakaribisha kwenye jumuiya kwa lengo la kuendeleza mtengamano sasa tunawaomba wasije wakasimamisha jumuiya nafahamu  kama nchi hatufanani kiuchumi kwa mazingira ya maendeleo lakini wajitahidi kutoa michango yao kwa wakati ili tuweze kwenda sawa.”amesema Millya.
Amesema kuwa, asilimia 61 ya bajeti iliyosomwa inapaswa kuchangiwa na nchi wanachama lakini mpaka leo wanaochangia kwa asilimia mia ni wadau wa maendeleo na  Mashirika mbalimbali .
Aidha ameomba  viongozi wakuu wa nchi zetu  wasaidie kusukumana huko juu ili watu wote wachangie  ili kufikia nyonzi ya kweli na kufikia malengo waliyojiwekea wasaidie  kusukumana huko  juu ili na wenzetu wachangie.
Naye Mbunge mwingine kutoka Tanzania     Dk.Abdullah Makame amesema bajeti iliyosomwa ni ndogo bado haikidhi majukumu ya mtengamano  kwani majukumu yameongezeka na jumuiya imepanuka  hivyo  kunahitajika  bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali.
“Hatutegemei  mabadiliko yoyote kiutendaji kwani bajeti hii ni  ndogo kulingana na majukumu ya mtengamano yaliyopo na  majukumu ya mtengamano yameongezeka hatutengemii kwa bajeti hii kitakuwa na mabadiliko yoyote ya kiutendaji”amesema Dk. Makame .
Aidha ameongeza changamoto  iliyopo ni kuwa bado nchi zetu hazijaweka vipaumbele  vya kutosha katika swala hilo jambo ambalo inapelekea bajeti kuwa ndogo .
Amesema kuwa ,Marais wa nchi hizo walielekeza mawaziri wa  nchi hizo kukaa pamoja na kupitia na kuangalia changamoto zilizopo katika nchi hizo na kufanya mapendekezo yao,hivyo nafikiri mawaziri hao  wakishakaa  watakuja na suluhisho kamili na kuweza kuinasua hali hiyo.