NA MWANDISHI WETU
KAMPENI ya Weka Akiba, Tumia na Ushinde kwa wateja wa akaunti nafuu, rahisi na salama ya NMB Pessa iliyokuwa na zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 250, imefikia ukomo kwa mkulima na mjasiriamali Emmanuel Amos Kakale wa Mitundu, Singida kuibuka na zawadi kuu ya Sh. Mil. 10.
NMB Pesa ambayo ni akaunti isiyo na makato ya mwezi inayofunguliwa kwa Sh. 1,000 tu, ilizinduliwa miezi mitatu iliyopita, ikiambatana na kampeni hii ambayo ilikuwa droo mbalimbali sambamba na matamasha makubwa katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.
Ukiondoa kitita hicho cha Sh. Mil. 10 kilichoenda kwa Kakale, droo ya fainali hiyo iliyofanyika Jumatano Mei 29, NMB Tawi la Mbezi Africana, ilishuhudia pia washindi wengine nane wakijinyakulia Sh. Mil. 3 kila mmoja, huku wengine wakitwaa mashine ya kufulia, TV janja (smart TV) na friji ya milango miwili.
Washindi wengine wa fainali hiyo iliyochezeshwa mbele ya Msimamizi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Irene Kahwili, walijishindia majiko ya gesi, bodaboda tano na pikipiki nane za magurudumu matatu maarufu kama Toyo.
Akizungumza kabda ya droo hiyo, Mkuu wa Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, alisema Kampeni ya Weka na Ushinde kupitia NMB Pesa ilipata mwitikio mkubwa ilipozinduliwa, hivyo kuifanya benki kutimiza lengo la kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki.
“Tulipata mwitikio mkubwa na tunaendelea kushukuru Watanzania wote waliotuunga mkono katika akaunti hii, ingawa tuna kila sababu ya kuendelea kuhamasisha Watanzania wenzetu kuzitumia akaunti hizi kwaajili ya kujiwekea akiba, nasi tunatumia nafasi hiyo kuwazawadia.
“Katika kampeni hii, tumekuwa na zawadi za kila wiki, kila mwezi na za fainali hii, ambako katika droo za kila wiki washindi 10 kwa wiki walijishindia Sh. 500,000 kila mmoja. Na kwa wiki tisa mfululizo tumekuwa tukitoa zawadi hizi kwa jumla ya washindi 90.
“Katika droo za mwezi, washindi watano kila mwezi kwa miezi miwili walijishindia Sh. Milioni 1 kila mmoja, ikiwa na maana tulishuhudia washindi 10 wakijinyakulia kiasi hicho kila mmoja, wakati kwenye matamasha yetu tulitoa zawadi za papo hapo zikiwamo pesa, pikipiki na majiko ya gesi,” alisema Donatus.
Alibainisha ya kwamba malengo ya benki yake na ahadi yao kwa Watanzania ni kuendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kidijitali na kupitia matawi yao 231 kote nchini, na hivyo kuendelea kuongeza idadi ya Watanzania kwenye Huduma Jumuishi za Kifedha, hasa walioko vijijini.
Donatus aliwataka wateja wa NMB na Watanzania kwa ujumla kuendelea na utamduni chanya wa kujiwekea akiba kupitia akaunti zao, kwani akiba ni jambo la msingi na lenye manufaa kwa mtu mmoja, jamii inayomzunguka na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kahwili – Mwakilishi wa GBT aliipongeza NMB kwa kampeni endelevu zinazolenga kukuza utamaduni chanya wa kujiwekea akiba, lakini zaidi kuwazawadia wateja wenye kufanya hivyo, jambo linalothibitisha namna inavyowajali na kuwapenda wateja wao.
“Kwa niaba ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), tunawahakikishia Watanzania ya kwamba kampeni na droo hizi zinazoendeshwa na NMB zinafanyika kwa kufuata vigezo na masharti yaliyowekwa na bodi hii yenye mamlaka ya kusimamia uendeshwaji wake kote nchini.
“Tuko hapa kuhakikisha kanuni hizo zinafuatwa katika kutafuta washindi na wenye bahati ndio watakaoshinda na hakuna ujanja ujanja,” alisema Kahwili mbele ya Meneja wa NMB Tawi la Mbezi, Lilian Riwa, wateja wa tawi hilo na waandishi wa habari.