Na. Damian Kunambi, Njombe
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amewataka watendaji kata pamoja na madiwani kuungana na ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyolenga kumtua mama ndoo kichwani kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji inayoletwa katika maeneo yao na kuhakikisha inakamilika na kotoa maji yaliyo safi na salama.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo katika jukwaa la wadau wa maji wilayani humo lililofanyika 05/05/2024 na kuhusisha Kamati ya Usalama, kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi,madiwani, maafisa Tarafa, watendaji kata pamoja na timu ya wataalamu (CMT) Wilayani humo.
“Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana wilayani kwetu kwani kwa sasa tuna miradi Saba ya maji yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 13.8 ambayo inaendelea kutekelezwa hivyo viongozi wa ngazi zote tunapaswa kusimamia fedha hizi ili zitumike ipasavyo na kuhakikisha miradi inatoa huduma stahiki”. Amesema Mwanziva.
Ameongeza kuwa jukwaa hilo limeandaliwa madhubuti ili kujadili na kuhoji changamoto zilizopo katika miradi mbalimbali na kuweza kuzitatua ili kuwaondolea wananchi changamoto zinazowapelekea kutembea umbali mrefu kufuata maji kwakuwa maji ni muhimu na hayana mbadala.
Aidha kwa upande wake Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Jeremiah Maduhu amesema kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025 wamepokea maelekezo kutoka serikalini yaliyo elekeza kuwa kipaumbele cha serikali ni kukamilisha miradi viporo.
Amesema sanjali na ukamilishaji wa viporo hivyo lakini pia RUWASA Wilayani humo imepokea kiasi cha Sh. Bilioni 1.30 ambapo kiasi cha Sh. Milioni 300 zitatumika katika uchimbaji wa visima na millioni 700 zitatumika kukamilisha baadhi ya miradi ambayo inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Ameongeza kuwa kuna haja ya kuboresha uunganishaji wa vyombo vya utoaji huduma za maji ngazi ya jamii (CBWSO) ili kuweza RUWASA kukidhi vigezo vya upataji fedha kiasi cha Sh. 50,000 kwa kila mtu ambaye atapata ufikiwaji wa chanzo kilichoboreshwa ikiwemo ujenzi mpya, upanuzi au ukarabati wa skimu ya maji ambapo kwa sasa wilaya hivyo bado haijakidhi vigezo vya upataji fedha hiyo.
Wise Mgina ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo lakini pia ni diwani wa kata ya Mundindi amewasihi madiwani wenzake kuweka usimamizi mzuri ili kuweza kupata fedha hizo kwani vijiji zaidi ya 60 vinapata maji na vinakidhi baadhi ya vigezo.
Hata hivyo kwa upande wao madiwani na watendaji mbalimbali walitoa mawazo mbalimbali yanayoweza kuboresha miradi hiyo huki wakiaahidi kusimamia vyema ili kuhakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika na yaliyo salama.