HALMASHAURI ya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi imetoa tuzo za elimu kwa shule za sekondari na msingi pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani mbalimbali.
Baada hivi karibuni kuonekana ufaulu umepungua katika wilaya ya Nachingwea hivyo uongozi umeandaa mikakati mingi mmoja wapo ni kutoka tuzo za kila mwaka za ufaulu ili kuongeza bidii na ufanisi bora kwa walimu pamoja na wanafunzi katika wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa utoaji tuzo hizo,mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa wameamua kuzirudisha tuzo hizo ili kutoa motisha na ushindani wa kimasomo baina ya shule moja hadi shule nyingine pamoja na ushindani wa wanafunzi na wanafunzi ambao utachangia kukuza elimu katika wilaya hiyo.
Moyo alisema kuwa ukitoa motisha kwa walimu basi ushindani wa kufaulisha utaongeza maana kila mwalimu anatamani shule yake na wanafunzi wake wafanye vizuri ili wapate tuzo jambo litakalo ongeza ufaulu.
Moyo alimalizia kwa kusema kuwa anataka kila mwaka wilaya ya Nachingwea iwe inashika namba moja katika mkoa wa Lindi na taifa kwa ujumla kama ilivyokuwa awali.
Kwa upande wake Afisa elimu msingi Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea,Stephen Urasa alisema kuwa tuzo hizo zinachangia kuongeza ushindani wa masomo kwa wanafunzi na shule zenyewe na kuleta matokeo chanya kwa ufaulu.
Urasa alisema kuwa tuzo hizo zitatolewa kila mwaka kwa wanafunzi watakao fanya vizuri na shule zitakazo faulisha vizuri kila mwaka.