Wananchi wa kata ya Kirumba mtaa wa Kabuhoro wametakiwa kulinda na kutoiba vifaa vya ujenzi kwaajili ya barabara ya Kabuhoro-Ziwani itakayojengwa kwa kiwango cha zege hivi karibuni na kuhakikisha wanawafichua na kuwafikisha katika vyombo vya dola wale wote watakaojihusisha na wizi au kuhujumu mradi huo.
Mbunge (MNEC) Mhe Dkt Angeline Mabula ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi mkandarasi eneo la kazi katika viwanja vya Bujumbura Kabuhoro ambapo amesema wizi wa vifaa vya ujenzi utasababisha barabara hiyo kujengwa chini ya kiwango pamoja na kuwataka vijana wa kata hiyo kutumia vyema fursa ya uwepo wa mradi huo kupata ajira na kujikwamua kiuchumi.
‘.. Udokozi usiwepo, mtakapodokoa saruji au kitu chochote mtaharibu barabara yenu, ukiwekwa pale kufanya kazi kuwa muaminifu, ukiwekwa pale fanya kazi uliyopewa, ukiwekwa pale uwe mlinzi wa rasilimali inayokwenda kuwepo pale’ Alisema.
Aidha Mhe Dkt Mabula amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa fedha za ujenzi wa mradi huo kupitia mfuko wa jimbo pamoja na kuwaasa wananchi wa kata hiyo kuhakikisha wanalipa fadhila kwa kumchagua kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu utakaokuja.
Kwa upande wake mkandarasi wa mradi huko ambae pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Kones Construction Ndugu Jerry Zadock licha ya kuahidi kutekeleza mradi kwa wakati, amesema kuwa atahakikisha anawatumia wakazi wazawa wa eneo hilo katika shughuli zote za ujenzi zisizohitaji taaluma kubwa na kuomba vijana wa eneo hilo kujitokeza kutumia nafasi hiyo pamoja na kuwaasa kufanya kazi kwa bidii pindi watakapobahatika kupata fursa hiyo kwani kumekuwepo na changamoto ya wazawa kuomba kazi na wakishapata wanakuwa wavivu katika kutekeleza majukumu yao huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano katika kipindi chote cha ujenzi.
Nae msimamizi wa mradi huo ambae ni wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA Mhandisi Gavdas Mliyuka amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi februari mwakani kwa kiwango cha zege ikiwa na urefu wa km 0.67 na mkandarasi ni kampuni ya MS Kones Construction kwa thamani ya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 275.
Wesa Juma ni diwani wa kata ya Kirumba ambapo amemshukuru Rais Dkt Samia na kumpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa ufuatiliaji na juhudi zake katika kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali jimboni ikiwemo na kata yake ya Kirumba.