Askari wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Songwe wametakiwa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia nidhamu, haki, weledi na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kauli hiyo imetolewa Februari 28, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP THEOPISTA MALLYA alipofanya baraza na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali.
Kamanda Mallya aliwapongeza askari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya mkoani humo na kuwataka waendelee kutoa huduma bora kwa Wananchi kwa kufuata Sheria, Kanuni, Misingi na Taratibu zinazoliongoza Jeshi la Polisi ili kuendelea kuwa kioo cha jamii kwa wananchi wanaowahudumia.
Pia, aliwataka Polisi Kata kuendelea kuwa karibu na wananchi na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuleta matokeo chanya ya kupunguza uhalifu na wahalifu katika jamii
Naye, Afisa Mnadhimu wa Polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP GALLUS HYERA amesisitiza Askari kutojihusisha na vitendo ambavyo vinaleta taswira mbaya kwa Jeshi la Polisi na kuwataka kufanya kazi kwa kufuata wimbo wa maadili ya Afisa wa Jeshi la Polisi ambao unasisitiza kutekeleza majukumu kwa kuzingaitia nidhamu, haki, weledi na uadilifu.
Mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa kukutana na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali mara kwa mara katika mabaraza na vikao kazi kwa lengo la kukumbushana majukumu ya kazi na kuweka mipango mkakati ya utendaji kazi ikiwemo kuzuia na kupambana na uhalifu.