Na Beda Msimbe, TBN, St. Petersburg, Urusi
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imejipanga kunufaika na soko la utalii la Urusi kwa lengo la kuliingizia taifa zaidi ya dola za Marekani milioni 500 kwa mwaka.
Zaidi ya wananchi milioni 13.4 wa Urusi husafiri na kutalii katika mataifa mbalimbali duniani. Kutokana na uwezo wao mkubwa wa matumizi ya kifahari, Tanzania inalenga kuvutia angalau asilimia moja ya watalii hao, sawa na watu 134,000, ambao wanaweza kuingiza zaidi ya dola za Marekani milioni 500 kwa mwaka.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru, wakati wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026) linaloendelea nchini Urusi.
Mafuru alisema kuwa katika mipango ya muda mrefu, TTB inalenga kuongeza idadi hiyo maradufu ndani ya miaka 10 ijayo ili kuiingizia Tanzania zaidi ya dola za Marekani bilioni moja kupitia sekta ya utalii.
Akiwa katika banda la Tanzania kwenye jukwaa hilo, Mafuru alisema anaendelea kufurahishwa na namna Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotekeleza kwa vitendo maono ya kutafuta wawekezaji na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa Watanzania.
Alisema ziara hizo zinazowahusisha viongozi na watendaji wakuu kutoka sekta muhimu kama miundombinu, utalii na madini zinaifanya diplomasia ya uchumi kuwa na matokeo chanya kwa taifa.
Mafuru amesema Tanzania imedhamiria kufungua kwa nguvu soko la Urusi kutokana na ukweli kuwa Warusi ni miongoni mwa watalii wanaotumia fedha nyingi zaidi duniani, hususan katika huduma za kifahari na anasa.
Aliongeza kuwa TTB imefanya tafiti mbalimbali na kubaini kuwa changamoto kubwa iliyokuwa ikiwazuia watalii wengi wa Urusi kuitembelea Tanzania ni umbali wa safari.
Hata hivyo, alisema kuanza kwa safari za moja kwa moja za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutapunguza muda wa safari na kuongeza hamasa kwa wananchi wa Urusi kuja kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania.
Aidha, Mafuru amesema umefika wakati kwa Watanzania kujifunza lugha ya Kirusi ili kuwavutia zaidi watalii kutoka nchi hiyo, kwani hupendezwa wanapopata huduma au kuongozwa kwa lugha yao ya nyumbani.
Akizungumzia Jukwaa la SPIEF 2026, Mafuru alisema ziara ya Rais Samia nchini Urusi imekuwa na mafanikio makubwa ambayo yanatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii pamoja na kuimarisha uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Urusi.
