Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said akijadili jambo na Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Dkt. Mzuri Issa katika kongamano la kujadili nafasi ya mwawake katika ngazi zamaamuzi lilifanyika Ukumbi wa Dkt.Shein ZURA Mjini Unguja .
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Zanzibar Khamis Abdulla akijadili jambo na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Tone Tinnes katika kongamano la kujadili nafasi ya mwawake na uongozi lilifanyika Ukumbi wa Dkt.Shein ZURA Mjini Unguja .
Mjumbe wa Mkutano Mkuu UVCCM Mkoa wa Mjini Zainab Saleh Salim akichangia katika kongamano la kujadili nafasi ya mwawake na uongozi lilifanyika Ukumbi wa Dkt.Shein ZURA Mjini Unguja .
PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO ZANZIBAR .
……..
Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar
Serikali zote mbili zitendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza mikakati maalum ya kuwawezesha wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi ili kuweka usawa wa kijinsia.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati wa kongamano la kujadili nafasi ya mwanamke na uongozi naibu wa Wizara hiyo Anna Athanas Paul amesema kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi inaonyesha wazi juhudi zinazochukuliwa na Saerikali hizo pamoja na kudumisha ,demokrasia Nchini.
Amesema nafasi zinazotolewa kwa wanawake si kwa upendeleo bali ni kwaajili ya kuziba mapengo yaliyoletwa na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia pamoja na kwenda sambamba na mifumo ya kuwandaa wanawake kuweza kuingia katika vyombo vya maamuzi.
Amesema historia inaonesha kuwa wanawake wengi waliachwa nyuma kutokana na mila na desturi zilizokua zikikandamiza haki zao hadi pale ilipotiliwa mkazo kitaifa na kimataifa na kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika vyombo hivyo.
Amesema adhma ya kufikia usawa wa kijinsia ni agenda inayotiliwa mkazo kimataifa hivyo aliwaomba wadau wa maswala hayo kuendeleza jitihada zao na kwenda sambamba na mifumo maalum ya kuwaendeleza wanawake ikiwa ni utekelezaji wa mikataba ya kikanda na kimataifa ili kuwawezesha wanawake kujitambua na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa katika Adhma hiyo.
Aidha aliwashukuru TAMWA ,PEGAO na ZAFELA kwa kutekeleza vyema mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL) kwa ufadhili wa Norway unaoendelea kutoa mafunzo kwa wanawake Unguja na Pemba ili kuwawezesha kugombania nafasi za uongozi kupitia vyama mbalimbali vya kisiasa.
Hata hivyo aliwataka wanawake hao kuzitumia vyema fursa za kuchagua na kuchaguliwa ili kupata haki yao ya kushiriki katika ngazi za maamuzi na kuleta maendeleo Nchini.
Kwa upande wake katibu Mkuu Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said alisema ipo haja kwa taasisi za Serikali na binafsi kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri kati ya wanawake na wanaume katika upatikanaji wa fursa mbalimbali za maenedeleo
Amesema wizara ya elimu ni miongoni mwa wadau wanaunga mkono juhudi za kupinga vitendo vya udhalilishaji kwani wameliweka suala la jinsia katika mitaala ya elimu na kubainisha kuwa wizara hiyo ni yakupigiwa mfano kwa kuweka usawa katika ugawaji wa nafasi za uongozi.
Aidha alifahamisha kuwa wizara hiyo inaendeleza jukumu la kuwawezesha wasichana kujitambua tangu msingi kupitia masomo mbalimbali ikiwemo ya uongozi maskulini.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari (TAMWA) Pemba Fat-hiya Said maesema kupitia mradi wa SWILL,wanawake wengi wameweza kujitokeza katika kugombania nafasi za uongozi ili kutimiza haki zao za kidemokrasia .
Amesema Dini ya Kiislamu haimzuwii mwanamke kushiriki katika masuala ya uongozi na vyombo vya maamuzi hivyo amewaomba kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kuweza kupata haki yao ya kuchaguwa na kuchaguliwa.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kongamano hilo Mjumbe wa Mkutano Mkuu UVCCM Mkoa wa Mjini Zainab Saleh Salim alisema matarajio yao ni kuongeza muamko kwa wanawake kuweza kupambania kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Kongamano hilo la siku moja limefanyika katika siku 16 za harakati za kupinga vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto likiwa na kauli mbiu “ungana wekeza kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.”