Mtendaji Mkuu wa Hazina SACCOS Bw. Festo Mwaipaja ametoa rai kwa wananchi kujiunga na SACCOS hiyo hasa wale ambao ni watumishi wa serikali kuu na serikali za mitaa TAMISEMI kwani taasisi hiyo imejikita kusaidia jamii hasa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu na kusaidia majanga kama misiba na magonjwa.
Hayo ameyasema leo Novemba 22, 2023 jijini Arusha katika maonesho ya wiki ya taasisi za kifedha yanayoendelea kwenye uwanja wa sheikh Amri Abed.
Amesema kumekuwa na mazao mapya ambayo yamelenga kugusa jamii moja kwa moja katika shughuli ambazo zinahitaji michango ya fedha .
“Katika hili Hazina SACCOS tumejikita kwenye maswala mbalimbali ya kijamii tuna mkopo wa elimu ambao unapatikana kwa gharama ya chini kuliko mikopo mingine ambapo tunatoa kwa asilimia 5 kama (Reducing Rate) ambayo ni Sawa na asilimia mbili”amesema
Akizungumzia mikopo kwa ajili ya msiba amesema mwanachama yeyote atakaepatwa na msiba ambao anapaswa kuwajibika anaweza kupatiwa mkopo utakaomsaidia kushughilikia gharama mbalimbali za msiba.
“Tumeshatoka kwenye ile dhama ya kuchangiana kidogo kidogo sasa hivi mwanachama wetu akipata msiba sisi tunawajibika katika majukumu mbalimbali ya msiba lakini pia kuna mkopo maalum wa mpaka shilingi milioni 3.000.000 ambao unatoka mapema ndani ya siku mbili mpaka tatu pindi tu tangazo la msiba litakapotolewa”amesema Mwaipaja.
Amesema mwanachama akipatwa na msiba kuna Bima ya rambi rambi ya mkono wa pole hivyo “Hazina SACCOS inawapa wanachama wake amani ya moyo wakati wowote wapatapo changamoto za kijamii.
Ameongeza kuwa wanajivunia mipango ambayo wameiweka ikiwemo mazao mapya ambayo yamejikita moja kwa moja katika kuinua na kusaidia wanachama wetu mara wapatapo changamoto mbalimbali zitakazowakabili, Karibu Hazina SACCOS upate amani ya moyo.