Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara imejipanga kuendeleza na kukuza ujuzi wa watendaji na wafanyakazi katika sekta ya utalii juu ya ukarimu na huduma bota nchini kwa ajili ya kupokea wageni wanaowasili kutalii nchini Tanzania.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo Novemba 10, 2023 wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga.
“Tutakuwa wakali kwa watu wasio na ukarimu mzuri kwa wageni wetu, hatutaki watu ambao kila mgeni anayefika wao wamenuna tu bila sababu, tutaendeleza mafunzo maalum na kwa hili nakipongeza Chuo cha Utalii kwani mmelifanya jambo hili la ukarimu kuwa kipaumbele chenu,” amesema Dkt. Abbasi.
Ametumia pia wasaa huo kueleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta hiyo kupitia Filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” ambapo amesema hadi mwezi Septemba watalii wameongezeka hadi kufikia watalii milioni 1.7 kwa watalii wanaotoka nje ya Tanzania na Pia mapato yameongezeka kutoka Dola Bilioni 1.3 hadi kufikia Dola Bilioni 3.1 na kuifanya sekta ya utalii kuzidi mauzo ya nje ya dhahabu iliyokuwa ikiongoza kwa miaka kadhaa katika kuingiza fedha za kigeni.