Rais wa Shrikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt Frank Walter Steinmeier akiweka shada la maua kwenye kaburi la pamoja la mashujaa 66 wa vita ya Majimaji waliouawa kikatili kwa kunyongwa na wakoloni wa kijerumani mwaka 1906.
Rais wa Shrikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt Frank Walter Steinmeier akizungumza baada ya kutembelea makumbusho ya Taifa ya Majimaji na kuzungumza na wahanga wa vita ya Majimaji ndani ya viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea.
Pichani mwenye nywele nyeupe ni Rais wa Shrikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt Frank Walter Steinmeier akiagana na watu mbalimbali kwenye viwanja vya makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea baada ya kukamilisha kazi kwenye makumbusho ya Taifa ya Majimaji na kuelekea katika shule ya msingi Majimaji mjini Songea.
…….
Na Albano Midelo,Songea.
Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt.Frank Walter Steinmeier amewafariji wahanga wa tukio la vifo vya mashujaa 67 waliua kikatili na wakoloni wa Kijerumani miaka 117 iliyopita mjini Songea mkoani Ruvuma.
Wakoloni wa kijerumani waliwauawa kikatili kwa kuwanyonga mashujaa wa vita ya Majimaji wapatao 67 wakiongozwa na Jemedari wa kabila ya wangoni Nduna Songea Mbano mwaka 1906 kisha kuwazika katika makaburi mawili ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Akizungumza baada ya kutembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea na kuzungumza na wahanga wa tukio hilo,Rais wa Ujerumani Dkt.Steinmeier amesema baada ya matukio ya vifo vya watu 67 yaliyotokea hapa Songea miaka 117 iliyopita, yeye kama Rais wa Ujerumani amepata fursa ya kukutana na wahanga kwenye eneo la tukio na kuwaomba msamaha kwa kilichotokea.
Amesema ameguswa na historia ya shujaa wa wangoni Nduna Songea Mbano na mashujaa wengine 66 ambao amesema historia yao ni ya kuhuzunisha sana hasa vifo vyao ambavyo waliuawa kikatili kwa kunyongwa.
“Leo baada ya kufika hapa Songea nimefahamu kuhusu jambo la kinyama walilotendewa mashujaa hawa limeendelea kuathiri familia nyingi hadi leo,ni watu wachache sana wanaofahamu historia hii nchini Ujerumani’’,alisisitiza Rais wa Ujerumani.
Amesema Mji wa Songea unawakilisha upinzani wa watanzania dhidi ya ukoloni wa kijerumani na kuongeza kuwa amefika Songea ili kubeba historia hiyo na kuipeleka kwa wajerumani wengi atakaporejea nchini kwake.
Hata hivyo amesema matukio yaliyotokea Songea miaka 117 iliyopita ni matukio yanayohusu jamii za nchi mbili za Tanzania na Ujerumani ambapo amesisitiza kuwa nchi ya Ujerumani lazima iwajibike kuhusu historia ya vita ya Majimaji ili kujenga kwa Pamoja Maisha ya siku za usoni.