Ngorongoro Crater, Arusha.
Majaji wakuu kutoka nchi za kusini na Mashariki mwa Afrika wameipongeza serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mh.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kuhifadhi eneo la Ngorongoro na hivyo kulifanya kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika.
Waheshimiwa majaji wametoa pongezi hizo leo tarehe 25.10.2023 walipotembelea Hifadhi ya Ngorongoro na kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo katika eneo hilo na kusema kuwa wamevutiwa na jinsi serikali ilivyoboeresha mazingira na kuimarisha uhifadhi.
Wakiongozwa na Mwenyeji wao Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, majaji wakuu hao waliweza kutembelea vivutio mbalimbali na kujionea uzuri wa Bonde la Ngorongoro na wanyama mbalimbali kama Faru, simba, tembo,viboko,nyati,pundamilia, ziwa Magadi na misitu inayopendezesha uwepo wa hifadhi hiyo.
Jaji Mkuu wa Namibia Mheshimiwa Peter Shivute alisema ziara yao katika eneo hilo imekuwa na tija kubwa na wamejionea jinsi serikali inavyosimamia uwepo wa hifadhi hiyo na kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka mataifa tofauti duniani.
“Tumefurahiswa na hifadhi ya Ngorongoro,kwa kweli serikali inafanya kazi kubwa ya kuhifadhi vivutio hivi,tangu tuingie Arusha tulikuwa na shauku kubwa ya kuja kujionea hali ya mambo ilivyo kwa kweli vinaifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya utalii”,alisema Jaji Mkuu Shivute kutoka Namibia.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zimbabwe mheshimiwa Luka Malaba alisema kufika kwake katika hifadhi hiyo amejionea jinsi sekta ya uhifadhi inavyopiga hatua na kuvutia watalii wengi kuingia nchini kujionea vivutio hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia urithi wa utamaduni na jiolojia Mhandisi Joshua Mwankunda amesema hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kusimamia ustawi wa vivutio vyote vilivyopo katika eneo hilo ili kuiwezesha serikali kupata mapato na kuboresha huduma za utalii na Moundombinu wezeshi kwa wageni wanaotembelea Hifadhi hiyo.
Mhandisi Mwankunda alisema uwepo wa hifadhi hiyo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na usimamizi bora na shirikishi kitu kinachosaidia watalii kutoka nchi mbalimbali duniani kufika na kujionea vivutio vilivyopo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama nchini Profesa Elisante Ole Gabriel alisema majaji wakuu hao walikuwa na shauku kubwa ya kufika eneo la Ngorongoro hasa kutokana na sifa iliyojijengea hifadhi hiyo katika nchi mbalimbali duniani.
Msafara huo ulihusisha zaidi ya majaji wakuu 150 kutoka nchi zilizopo Kusini na Mashariki mwa Afrika ambao walikuwa jijini Arusha kuhudhuria Mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Majaji wakuu wa nchi hizo.