Mkurugenzi wa Shule ya Mchepuo wa kiingereza ya Enyorata Pre &Primaryhiyo, Agness Laizer akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.

Mwalimu wa Shule ya mchepuo wa kiingereza ya Enyorata Pre &Primary Godlove Urio akizungumza kiwango cha ufaulu shuleni hapo.

Wahitimu wa darasa la saba wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Mahafali ya pili shuleni hapo .
…….
Julieth Laizer ,Arusha .
Serikali imeombwa kuzisaidia shule binafsi kwa kuzipatia vitabu vya kujisomea kwani vilivyopo havitoshi kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule hizo.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Enyorata Pre &Primary iliyopo mkoani Arusha ,Agness Laizer wakati akizungumza katika mahafali ya pili ya darasa la saba ambapo jumla ya wanafunzi 25 walihitimu masomo yao.
Agnes amesema kuwa , shule hizo za binafsi zimekuwa zikifanya vizuri katika kuiunga mkono serikali katika juhudi mbalimbali za maendeleo hivyo nazo zinapaswa kusaidiwa na serikali kwani wote kwa ujumla wanafanya wajibu mmoja wa kusaidia swala la maendeleo.
Amesema kuwa, wanaiomba serikali iwasaidie kuwapatia vitabu vya kujisomea kwani wana upungufu mkubwa wa vitabu hivyo kwa ajili ya kuinua kiwango cha elimu shuleni kwa wanafunzi na hata walimu pia.
“Unajua unapokuwa na vitabu vya kutosha shuleni unamrahisishia mwalimu kuweza kufundisha vizuri darasani kwani kila mwanafunzi anakuwa na kitabu chake wakati mwalimu akifundisha na hivyo kumfanya mwanafunzi kuelewa zaidi .”amesema .
Aidha Agness amesema kuwa ,shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 402 na changamoto nyingine wanayokabiliana nayo shuleni hapo ni ubovu wa barabara kutoka Nadosoito hadi Dampo hasa kipindi cha mvua imekuwa ni ngumu magari kupitika na kufanya wanafunzi kuchelewa kufika darasani kwa wakati kutokana na hali hiyo.
Aidha wameomba serikali kuwatengenezea barabara hiyo ili iweze kupitika kwa haraka na kuondokana na changamoto mbalimbali za wanafunzi kuchelewa masomo hasa kipindi cha mvua.
Aidha amesema kuwa, shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika taaluma ambapo tangu shule ianzishwe mwaka 2015 kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kimezidi kuongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka jana walihitimu wanafunzi 13 na walifaulu wote na kwa mwaka huu wanategemea watoto wote 25 watafaulu kutokana na ufundishaji mzuri unaofanywa na walimu hao.
Aidha amesema kuwa, shule hiyo ambayo imezungukwa na jamii ya kifugaji wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibadilisha jamii hiyo kielimu na kuwafanya wazazi kuwa na mwitikio mkubwa wa kuwapeleka watoto wao shuleni tofauti na hapo awali walikuwa wakiishia kuchunga tu.
Kwa upande wa mgeni rasmi ,Mmisionari Ozney Dakrusu amewataka wanafunzi hao kwenda kujiendeleza zaidi kimasomo na wasibwete kwani ndio kwanza elimu imeanza huku akiwataka kusoma zaidi ili kufikia ndoto zao.
Aidha amewataka wazazi kuwa kipaumbele kuendeleza ndoto za watoto wao badala ya kuwakwamisha kufikia malengo yao kwani baadhi ya wazazi wengi wamekuwa ni kikwazo kikubwa kwa watoto wao kushindwa kufikia malengo yao.
Naye Mwalimu Godlove Urio akizungumza katika mahafali hayo amewataka wanafunzi kuiwakilisha vyema shule hiyo katika mitihani ya darasa la saba huku akiwataka kuepukana na makundi yasiyofaa pindi watakapokuwa mtaani wakisubiri matokeo yao.
Aidha amewataka wazazi mbalimbali hususani wanaozunguka shule hiyo ikiwemo jamii ya kimasai kuwaleta kwa wingi watoto wao shuleni hapo ili waweze kupata elimu na kuwa viongozi bora wa baadaye.
Baadhi ya Wanafunzi waliohitimu, Robson Urio na Aisha Kibaha wameshukuru shule hiyo kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa elimu bora kwao na kuweza kuwaandaa vyema katika mitihani ya kumaliza darasa la saba huku wakiahidi kuitangaza vyema shule hiyo katika mitihani yake.
Mwisho.