Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamapuli, wakiwa nje ya ofisi za MAMLAKA ya hifadhi ya Taifa Katavi, Sitalike Mkoani
Na. Zillipa Joseph, Katavi.
Watanzania wametakiwa kuona umuhimu wa kufanya utalii wa ndani na kujionea vivutio vilivyopo katika mbuga zetu ili kuweza kubadili mfumo wa maisha.
Rai hiyo imetolewa na bwana Gwamaka Bukuku ambaye alikuwa Mratibu wa safari ya utaliii iliyofanywa na wanafunzi na walimu wa Mwamapuli Sekondari na baadhi ya wakazi wa Maji Moto katika halmasahuri ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Bukuku alileleza kuwa kutembelea hifadhi kunasaidia kufahamu maisha ya viumbe mbalimbali wakiwemo wanyama pori hali ambayo anaamini watanzania wakiona ufahari huo wataacha tabia za kuvamia misitu na kuharibu vyanzo vya maji.
Aliongeza kuwa uharibifu katika vyanzo vya maji ikiwemo mito inayotirisha maji kuelekea katika hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo wananchi wamekuwa wakichepusha maji ya kito kwa ajili ya kilimo cha mpunga una athari kubwa kwa wanyama kama viboko ambao maisha yao wanatumia muda mwingi zaidi katika maji.
Alisema lengo la safari hiyo ni kuwapa fursa ya kujifunza hasa wanafunzi ambao ndio watu wazima wa baadae waone umuhimu wa hifadhi zetu sanjari na kujifunza utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi walisema wamefurahi kushiriki katika safari hiyo kwani wamewaona wanyama wengi pamoja na kujifunza namna wanyama mbalimbali wanavyoishi.
Kwa upande wake mwalimu Julius Sanga aliiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kutoa elimu ya manufaa ya utalii wa ndani kwa Watanzania ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani hali itakayosaidia kuelewa umuhimu wa utunzaji wa mazingira na mali asili tulizo nazo.
Mwl. Sanga alisema endapo wananchi wengi watakuwa na uelewa wa umuhimu wa utalii watachukua hatua dhidi ya waharibifu wa mazingira hasa wafugaji wanaoingiza mifugo kuchungandani ya hifadhi.
Bi. Faith Kalenge ni mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwamapuli alisema waliamua kuwapeleka wanafunzi kufanya utalii ili wawe chachu katika jamii ya kuenzi hifadhi za Taifa.
‘Hawa ni wanafunzi wa kutoka jamii tofauti tofauti, wungine I watoto wa wafugaji. Tumewaleta huku kwa makusudi ili wajifunze maisha ya wanyama na wawe chachu ya mabadiliko kwa jamii’ alisema.