Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo akizungumza na mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa MRRH.
Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazahura akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi (Echocardiograph – ECHO) mtoto wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH).
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Loveness Mfanga akimsikiliza mwananchi wa mkoa wa Kilimanjaro akijibu maswali ya ufahamu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH)Picha na: JKCI
Na: Mwandishi Maalum – Kilimanjaro2
Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani wameishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufikisha huduma za kibingwa za matibabu ya moyo mkoani Kilimanjaro.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) wananchi hao wamesema uhitaji wa matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo mkoani humo ni mkubwa.
Elishadai Kimaro mkazi wa Kilimanjaro alisema kutokana na wingi wa watu kutoka mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani idadi ya watu wanaohitaji matibabu ya moyo toka kambi hiyo kuanza imekuwa kubwa hivyo watu kurudishwa nyumbani na kurejea tena siku inayofuata.
“Ninaiomba Serikali huduma za matibabu ya moyo hapa mkoani kwetu zifanyike mara kwa mara au ikiwezekana tuwe na hospitali yetu inayotoa huduma hizi za matibabu ya moyo, kambi maalum ya siku tano na baadaye wataalamu kuondoka haitoshelezi kufikia mahitaji ya wanakilimanjaro”, alisema Kimaro.
Kimaro alisema kupitia kambi hiyo amepata nafasi ya kuchunguza afya ya moyo wake kwani alikuwa na hofu ya kuwa na matatizo ya moyo lakini hakujua ni nini afanye hadi hapo aliposikia ujio wa madaktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete hivyo naye kutumia fursa hiyo kupima.
Twaha Masawe mkazi wa Kilimanjaro alisema huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa afya kutoka JKCI amezipenda kutokana na watoa huduma wanavyozungumza vizuri na wagonjwa na kuwapa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Masawe alisema kupitia kambi hiyo ameelimishwa kutokuacha kutumia dawa za shinikizo la damu na kama ataacha anaweza kupata madhara katika moyo wake ama kupata kiharusi.