Pix 1. Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Vickness Mayao akizungumza wakati wa kikao kazi cha mawasilisho ya Mfumo wa kidigitali kwa wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kilichofanyika Agosti 21, 2023 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali akizungumza wakati wa kikao kazi cha mawasilisho ya mfumo wa kidigitali kwa wajumbe wake kilichofanyika Agosti 21, 2023 jijini Dodoma.
Kiongozi wa Timu ya kuboresha mfumo wa kidigitali wa kutoa taarifa za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali,
Dkt. Richard Sambaiga akitoa taarifa kuhusu mfumo wa kidigitali kwa Wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakati wa kikao kazi cha kupitia mfumo huo kwa Wajumbe wa Baraza la Taifa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kilichofanyika Agosti 21, 2023 jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakishiriki katika kikao kazi
cha mawasilisho ya mfumo wa kidigitali kilichofanyika Agosti 21, 2023 jijini Dodoma.(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM).
…………
Witness Masalu ,WMJJWM Dodoma.
Wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) wametakiwa kuwa mabalozi wa kutoa elimu kuhusu mfumo wa upatikanaji wa taarifa za Mashirika hayo ili isaidie Serikali na wadau mbalimbali kutambua mchango wa NGOs katika jamii.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Dkt. Lilian Badi wakati wa mafunzo ya mfumo huo
kwa wajumbe wa NACONGO yaliyofanyika jijini Dodoma Agosti 21,2023.
Dkt. Lilian amewaasa wajumbe hao kuchota maarifa na kwenda kuirahisishia jamii kuelewa namna ambavyo mfumo huo unatumika kwa kupata taarifa muhimu hasa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayowagusa wananchi.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuja na mfumo wa kurahisisha upatikanaji wa taarifa ili kuleta uwazi na uharaka wa taarifa za Mashirika Yasiyo ya kiserikali, hivyo sisi tukiwa kama wawakilishi wao kutoka mikoa yote nchini ni jukumu letu kuhakikisha tunaenda kujibu maswali yao kwa kutumia ujuzi tutakaopata hapa” amesema Dkt. Badi.
Naye Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao ameeleza kwamba taarifa zitazopatikana katika mfumo huo si taarifa zote bali ni taarifa za msingi juu ya mashirika husika ambazo zitawezesha wadau kulingana na mahitaji yao.
“Kigezo cha mipaka ni muhimu na kimezingatiwa kwenye mfumo huu kwani kuna taarifa ambazo ni nyeti na si za kuonwa na kila mtu hivyo mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa taarifa zote muhimu tu zilizolengwa kuwafikia wadau ” amesema Vickness.
Kwa upande wake Kiongozi wa timu inayoboresha mfumo huo Dkt. Richard Sambaiga amesisitiza kuwa mfumo huo si mpya bali ni mfumo uliokuwepo na lengo lake ni kuboresha huduma ya upatikanaji wa taarifa kwa wadau kutoka pande zote tofauti na awali ambapo mfumo ulikuwa unatumika na Ofisi ya Msajili peke yake.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imeendelea kutoa mafunzo juu ya mfumo wa taarifa za mashirika hayo mfumo ambao upo mbioni kukamilika ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wadau wote.