Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema, wadau wa habari wangependa ukamilifu wa uundwaji wa kanuni za habari usivuke mwezi Oktoba mwaka huu.
Balile alitoa kauli hiyo tarehe 17 Agosti 2023, alipozumgumza na baadhi ya wanahabari katika ofisi za jukwaa hilo, jijini Dar es Salaam.
Alisema, mwenye jukumu la kusimamia na kukamilika kwa kanuni ni Waziri wa Habari, Mawasiliano n Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
“Tungependa kanuni za habari zipatekane mpaka kufika Oktoba, hili ni ombi kwa kuwa, Waziri wa Habari (Nape Nnauye) halazimishwi na sheria kuhusisha wadau.
“Ni kutokana na utaratibu wake wa kushirikisha wadau ndio maana anafanya hivyo, wala safari hii suala la kanuni za habari halipelekwi bungeni, linaishia kwa kwake Waziri Nape,” alisema.
Balile alisema, baada ya bunge kupitisha marekebisho ya sheria ya habari, kinachofuata sasa ni kuomba fursa ya kukutana na serikali kwa ajili ya kupendekeza mambo gani yaingie kwenye kanuni.
Alisema, miongoni mwa mambo ambayo wadau wa habari wangependa kuona yanaingia kwenye kanuni mpya na kuanza kutumika ni pamoja na suala la leseni ya magazeti kuwa zaidi ya miaka mitano tofauti na ilivyo sasa.
“Tutashauri serikali kwamba, kanuni zetu zielekeza kuwa lesini pamoja na kitambulisho cha mwanahabari (press card), zidumu kwa zaidi ya miaka mitano,” alisema na kungeza.
“Makosa ya kitaalumu yanapaswa kubaki kwa wanataaluma wenyewe, hili litasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza mlundikano wa kesi mahamani.”
Kwenye mkutano wake na wanahabari Balile alisema, eneo lingine wanalotarajia liingie kwenye kanuni, ni umiliki wa hisa katika vyombo vya habari kutowekewa mipaka.
Alisema, sio jambo rahisi kwa mwekezaji kutoka nje awekeze kwenye vyombo vya habari halafu asiwe na sauti, huku akitoa mfano wa uwekezaji wa bila kiwango cha asilimia katika maeneo mengine ikiwemo mitandao ya simu.
“Sheria inataka mwekezaji kutoka nje ya nchi amiliki hisa isiyozidi asilimia 49, jambo hili linapunguza uwekezaji kwenye vyombo vya habari.
“Tutamshauri Waziri Nape kwamba, mwekezaji kwenye vyombo vya habari asiwe na ukomo kama ilivyo kwenye mitandao ya simu na maeneo mengine,” alisema Nape.
Pia alisema, miongoni mwa sehemu ya sheria ya sasa inaruhusu mwandishi wa habari kumshitaki mtoa taarifa endapo atakataa kutoa taarifa inayotakiwa na mwanahabari.
“Hili lieleweke vizuri, kuna maofisa wa serikali ambao wakitakiwa kutoa taarifa kwa wanahabari, wanagoma kufanya hivyo. Kwa sheria ya sasa, mwanahabari anaweza kumburuza mahakamani ofisa ambaye hatotoa taarifa inayotakiwa,” alisema Balile.
Pia Balile amemshukuru Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), kwa kuingilia kati katika maeneo ambayo maofisa wa serikali walipotaka kunyanyasa wanahabari.
“Kuna maofisa wa serikali walitaka kuendeleza utamaduni wa kunyanyasa wanahabari. Jambo hili limekuwa likiwatesa wengi, lakini nimshukuru Msigwa maana amekuwa makini katika hili,” alisema Balile.