Mmiliki wa Hospitali ya E.M Dkt, Egina Makwabe
Dkt. Makwabe akielezea namna mashine yakusafishia damu inavyofanya kazi
Hospitali ya E.M iliyopo Mjimwema, Kigamboni
Duka la dawa katika hospitali ya E.M
………………………………………………..
Na Sidi Mgumia, Dar Es Salaam
Timu ya watoa huduma za afya kutoka Hospitali ya E.M iliyopo Mjimwema wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam, imedhamiria kutoa huduma bora na za kisasa kwa watu wengi bila kujali uwezo.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na mmiliki wa hospitali hiyo Dkt. Egina Makwabe alipofanya mahojiano maalumu na mwandishi wetu alipotembelea hospitali hiyo mpya na ya kisasa yenye hadhi na viwango vya hospitali ya mkoa, iliyofunguliwa Machi 27, mwaka huu.
Dkt.Makwabe amesema kuanzishwa kwa hospitali hiyo ya kwanza ya binafsi kwa ngazi ya mkoa ndani ya wilaya ya Kigamboni ni namna mojawapo ya kutoa suluhu ya changamoto za upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
“Tumechagua kuleta huduma bora na za kisasa Kigamboni na Dar es salaam kwa ujumla, tutahakikisha huduma zetu zinatolewa kwa weledi mkubwa kwasababu tulifanya uchunguzi na tukagundua wilaya hii inahitaji huduma za afya za kibingwa.
“Tuligundua kuwa hakukuwa na hospitali yoyote ya binafsi ya ngazi ya mkoa na wagonjwa walikuwa wanalazimika kwenda mbali na Kigamboni kufuata huduma za matibabu,” alisemaDkt.Makwabe
Aliongeza kuwa lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanawafikia watu wengi na kwa wakati, huku wakizingatia kuwa dunia yasasa imebadilika kwenye vifaa vya kisasa na teknolojia za hali ya juu, mabadiliko hayo yanawafanya na wao kuhakikisha wanakwenda na kasi hiyo.
“Pamoja na kuwekeza fedha nyingi hapa, lakini sisi ni watoa huduma, moja ya malengo yetu ni kuhakikisha tunakuwa na tija kwa watu walio tuzunguka bila kujali uwezo wao.
“Tunajipanga ili kuona njia sahihi ya kusaidiana na wananchi waliotuzunguka, hatutaacha kumtibu mtu kwasababu hana uwezo, kama unaweka hospitali kama hii na umezungukwa na watu ambao hawana uwezo wa kuzipata huduma zako haitaleta maana kwao,” alisisitiza Dkt. Makwabe
Alisema ilikufanikisha utaratibu wa kutoa huduma hata kwa wasio na uwezo wanatarajia kuanzisha mfuko ambao utabeba gharama za kuwachangia wasio na uwezo.
Pamoja na mambo mengine Dkt.Makwabe amesema pamoja na kuwapo kwa changamoto ya madaktari bingwa nchini, lakini hospitali ya EM imejipanga kwenye eneo hilo kwani inao wataalamu wa kutosha.
“Katika hospitali nyingi za serikali na binafsi hapa nchini kuna changamoto za madaktari, lakini kwetu hali ni tofauti tunao madaktari bingwa lakini katika hospitali hii tumejitahidi kuweka madaktari bingwa 13, kati yao wapo madaktari wa watoto, wakina mama, daktari wa magonjwa ya ndani, figo na upasuaji wa aina zote.
Dkt. Makwabe ameweka wazi kuwa hospitali yake imejipanga vilivyo kutoa huduma zote za kibingwa na zisizo za kibingwa zikiwemo huduma za kusafisha damu, huduma za X-Ray, CT-Scan, maabara kubwa, duka kubwa la dawa, matibabu ya meno, macho, masikio, koo, huduma za upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za kulaza, kuhudumia wagonjwa wa nje, matibabu ya mapafu, vidonda vya tumbo, magonjwa ya ngozi pamoja na huduma za wakina mama na watoto.
Kwa upande mwingine Dk Makwabe ameishukuru sana Serikali kwa ushirikiano alioupata kuanzia hatua ya kwanza hadi walipofikia sasa na ana amini ushirikiano huo mzuri utaendelea.
Pamoja na mambo mengine, ameishauri Serikali kupunguza urasimu kwenye baadhi ya mambo yakiwemo ya usajili wa vituo ambao umekuwa ukicheleweshwa bila sababu.
“Ni vyema Serikali ikarahisisha zoezi la usajili wa vituo binafsi, vituo vikiwa vimeshakamilika kabisa serikali kupitia vyombo vyake husika ifanye usajili mapema, watu waweze kuendelea na kazi, kukawia kusajili kunawagharimu sana wawekezaji kwasababu muda ambao wanasubiri usajili wao wanakuwa tayari wameshaweka wafanyakazi ambao wanalipwa mishahara bila kuzalisha chochote.
Inaumiza sana, kituo kikiwa kimekamilika na kinamaliza miezi sita au mwaka hakijasajiliwa ni tatizo kubwa kweli kweli,” aliongeza Dkt. Makwabe
Dkt. Makwabe ameomba kuwe na ushirikiano wa vitendo kati ya serikali na sekta binafsi, kama vile kubadilishana wagonjwa hasa katika maeneo ambayo hospitali binafsi hazina uwezo wa kuwahudumia au hospitali za serikali hazina uwezo, ni vema kukawa na utamaduni wa kushirikiana kivitendo.
“Kama katika hospitali hii hakupatikani huduma fulani basi waweze kuwapeleka wagonjwa kwenye hospitali za serikali ili watibiwe bila kupata kikwazo chochote na walioshindikana katika hospitali za serikali waelekezwe kwenye hospitali binafsi bila vikwazo.”
“Ikumbukwe tu kuwa sekta binafsi inavyowekeza kwenye afya inaipunguzia serikali mzigo mkubwa, hivyo kuwe kuna namna ya kusaidiana katika matumizi ya vifaa tiba kama vile mashine za MRI na nyinginezo, badala yakupatikana mashine nne kwenye eneo dogo ni vema zikatawanywa katika maeneo mbalimbali, lakini hili litafanikiwa kama kutakuwa na ushirikiano wa kitabibu kati ya serikali na Sekta binafsi,” alisema Dkt. Makwabe
Akizungumzia wazo la kujenga hospitali hiyo katika wilaya ya Kigamboni, alisema kuwa imekuwa ni ndoto yake ya muda mrefu tangu akiwa chuo, hivyo amefurahi kwakua ndoto yake ya kutenda jambo jema la kuweka kumbukumbu kwa taifa imetimia.
“Ninashukuru kuwa watu wameipokea huduma vizuri na tuko katika hatua za mwisho kukamilisha suala la matumizi ya bima za afya, tunaamini kuwa hii itatupa nafasi ya kuwahudumia watu wengi zaidi, kila kitu kitakuwa sawa ndani ya muda mfupi na huduma zitaendelea kutolewa kwa ufanisi mkubwa kwa kuzingatia taratibu zote muhimu za utoaji wa huduma za afya nchini,” alisema Dkt. Makwabe
Hospitali ya EM ilianza kujengwa Disemba 2019, ilipofika 2020 ujenzi ulilazimika kusimama kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona, Aprili 2022 ujenzi uliendelea hadi kufunguliwa.