Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) ni Taasisi iliyodhamiria kutoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uelewa wa namna inavyotimiza majukumu yake ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini,Mafuta na Gesi Asilia kwa mujibu wa Sheria.
Majukumu wanayoyasimamia kwa mujibu wa Sheria, ni pamoja na kuweka wazi taarifa za Mapato ya Serikali na malipo ya Kodi yanayotoka kwenye Kampuni za Madini,Mafuta na Gesi Asilia kwa Umma ili kuhamasisha Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali hizo.
Ndio maana TEITI wameamua kushiriki kwenye Maonesho ya tano ya Teknolojia ya Sekta ya Madini yanayofanyika Mkoani Geita ili kukutana na wananchi moja kwa moja na kuzungumza nao kwa kuwapa elimu juu ya kazi zinazotekelezwa na Taasisi hiyo.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Nyanh’wale David William aliyetembelea katika Banda la TEITI kwenye Maonesho hayo, Afisa Msimamizi wa Fedha wa Taasisi hiyo Erick Ketagory amesema kuwa wananchi wana haki ya msingi kwa mujibu wa Sheria kupata taarifa zote muhimu za Mapato ya Serikali na malipo ya Kodi yanayotoka kwenye Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia.
“Taasisi hii ina wajibu mkubwa wa kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia. Ndio maana sisi tuko hapa kutoa elimu kwa wananchi ili wafahamu kuwa wanao wajibu wa kupata taarifa hizi kwa usahihi” ameeleza Ketagory.
Taasisi hiyo imeundwa kwa Sheria namba 23 ya TEITA ya mwaka 2015 ambayo imeunda Kamati ya Uwazi na Uwajibikaji (Kamati ya TEITI) yenye wajumbe nane(8) inayoongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu Ludovick Utouh ambapo kazi za kila siku za TEITI zinatekelezwa na Katibu Mtendaji.