Rais wa chama cha madaktari Tanzania (MAT),Dk Shadrack Mwaibambe  akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha .
Daktari wa afya ya kinywa mkoa wa  Arusha,Dk Omar Chande akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha.
Baadhi ya madaktari hao wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa chama hicho katika mkutano unaoendelea jijini Arusha.
………………………………
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari juu ya mlipuko wa  janga la Ebola  ambao unaripotiwa kutokea nchi jirani ya Uganda huku wakitakiwa  kuondokana na safari zisizo  za lazima ili kuepukana  na ugonjwa huo. 
Hayo yamesemwa   jijini Arusha  na Rais wa chama cha madaktari Tanzania (MAT),Dk Shadrack  Mwaibambe wakati akizungumza katika mkutano  wa 54 wa chama hicho unaofanyika  jijini Arusha.
Dk. Mwaibambe amesema kuwa ,kutokana na kuwepo kwa mlipuko huo  jamii inatakiwa kuelimishwa mapema kuchukua tahadhari ikiwemo  kuepukana na safari zisizo za lazima kwenda nchini Uganda.
“Kumekuwepo na muingiliano mkubwa sana wa wananchi kwenda nchi jirani kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwani Uganda hapo  sio mbali ni kilometa  mia mbili  kutoka mpaka wa Tanzania ,hivyo ni lazima kila  mmoja  wetu atoe elimu ya kutosha ili wananchi waweze  kuchukua tahadhari mapema  “amesema  Dk Mwaibambe .
Dk. Mwaibambe amesema kuwa,kutokana na kuripotiwa kwa ugonjwa huo nchini Uganda ni muhimu  serikali ikachukua  tahadhari mapema ili ugonjwa huo usiingie  nchini kwetu na kuweza kuleta  madhara .
“Kutokana na ugonjwa huo ni vizuri tahadhari ikachukuliwa kwenye viwanja vya ndege kwa kuwakagua  watu wanaoingia na watakaogundulika  kuwa na ugonjwa huo  wawekwe  garanteeni  ili ugonjwa usiingie  nchini kwetu na kwa kufanya  hivyo tutaweza  kudhibiti kwa kiwango  kikubwa  sana.”amesema Dk Mwaibambe .
Amesema kuwa ,katika mkutano huo watajadili  agenda ya  umuhimu wa  kupata chanjo ya pili  ya uviko 19 kwa wale watu  ambao hawakupata awamu  ya kwanza  ili waweze kupata awamu ya pili sambamba na kujadili  namna ya kuchukua  hatua katika kudhibiti  ugonjwa wa Ebola  .
Kwa upande wake  Rais  mstaafu wa chama cha madaktari Tanzania,Dk Elisha Osati amesema kuwa,  kutokana na kuwepo kwa mlipuko wa  ugonjwa wa  Ebola  ulioripotiwa  nchini Uganda ni wajibu wa kila  mmoja  wetu  kuweza kuchukua tahadhari  za haraka  hususani katika mipaka yetu  kuhakikisha ugonjwa huo  hauingii  hapa  nchini  kwetu.
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanafuata masharti  yanayotolewa na wataalamu namna ya kupambana na ugonjwa huo wa Ebola  .
Kwa upande wake  Daktari wa afya ya kinywa  mkoa wa Arusha,Dk Omar Chande amesema kuwa,ni vizuri chama cha madaktari Tanzania kuendelea kuongeza nguvu zaidi katika  kuhamasisha utoaji wa chanjo ya uviko 19 kwenye vituo vya afya ili  watu wote wapate muhamko wa chanjo hiyo.
Aidha amewataka wadau mbalimbali kutoa elimu ya kutosha  kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari  kuhusu ugonjwa huo ili usiweze kuingia huku nchini.