Mwonekano wa banda la TFRA wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Ushirika Duniani yanayofanyika kitaifa mkoani TaboraNaibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde (wa pili kulia) na wajumbe walioambatana nae wakimsikiliza Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Kati Joshua Ng’ondya walipotembelea banda hiloNaibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akiangalia sampuli mbalimbali za mbolea katika banda la TFRA wakati wa maadhomisho ya siku ya Ushirika Duniani na kuelezwa matumizi ya mbolea hizo na Kaimu Meneja kanda ya kati Joshua Ng’ondya
………………….
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuwahimiza wakulima kujiunga katika vyama vya ushirika kwani vyama hivyo huleta matokeo chanya katika kukuza uchumi wa mtu mmoja moja na jamii kwa ujumla.
Naibu Waziri Mavunde ametoa wito huo jana tarehe 28 June, 2022 akifungua Siku ya Ushirika Duniani (International Cooperative Alliance) kwa mwaka 2022 ambayo Kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Maonesho ya Nanenane vilivyopo Ipuli Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora na yatadumu kwa siku tatu kuanzia Tarehe 28 Juni hadi tarehe 02 Julai, 2022.
Pamoja na wito huo, Mavunde ameitaka TFRA kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima pamoja na kudhibiti ubora wa mbolea ili kilimo kinachofanywa na watanzania kiwe na tija na kuchangia katika kupunguza utegemezi.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa kilimo inamkakati wa kukuza sekta ya kilimo kwa 10% ifikapo mwaka 2030 ikiwekeza katika masuala ya Utafiti na Umwagiliaji huku bajeti ikipanda kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 294 hadi kufikia Bilioni 954 kwa mwaka wa Fedha 2022/2023.
Akielezea majukumu ya TFRA kwa Mgeni Rasmi na Waziri wa Kilimo Mavunde, Kaimu Meneja TFRA Kanda ya Kati Joshua Ng’ondya alieleza kuwa shughuli zinazotekelezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini ni pamoja na kusimamia na kudhibiti ubora wa mbolea, usajili wa mbolea, usajili wa wauzaji wa mbolea na ukaguzi wa mbolea.
Majukumu mengine ni kudhibiti utengenezaji, uingizaji na biashara ya mbolea nchini, kusimamia na kutoa bei elekezi kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini kwa kuzingatia gharama ya kununua na kuingiza mzigo nchini pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wa mbolea juu ya Sheria, Kanuni na taratibu zinazosimamia tasnia ya mbolea.
Akielezea mahitaji ya mbolea kwa mikoa ya Tabora na Kigoma kwa mwaka ni tani 108,866 na kufafanua kuwa ofisi yake imetoa mafunzo ya matumizi na biashara ya mbolea kwa wafanyabiashara na wauzaji wa mbolea 591 na Wanachuo 81 cha MATI Mubondo juu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani huadhimishwa kila jumamosi ya kwanza ya mwezi Julai kila mwaka Duniani kote ambapo jamii ya wanaushirika hujumuika na wanajamii wengine na wadau wa maendeleo ya ushirika kusheherekea siku ya ushirika duniani.
Lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutangaza shughuli za wanaushirika, kujadili mafanikio na changamoto zilizopo kupitia ushirika na kupanga mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo, kupanua wigo wa ushirikiano na wadau wa ushirika kitaifa na kimataifa.