Na. Damian Kunambi, Njombe
Kaimu katibu tawala wa wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Linus Malamba ameagiza kukamatwa kwa mzabuni aliyefahamika kwa jina la Michael Lameck kutokana na kutopeleka vifaa vya ujenzi kwa wakati na kupelekea kuzorota kwa mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo unaoendelea katika shule ya msingi Lusala iliyopo katika kata ya Lupanga wilayani humo.
Malamba ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF ikiwemo mradi huo wa Lusala kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere ambapo alipofika Lusala alikuta maendeleo si mazuri huku ikielezwa kuwa mzabuni ndiye kikwazo.
Kwa mujibu wa viongozi wa kata na kijiji cha Lusala akiwemo diwani Dominicus Mganwa wamesema kuwa mzabuni huyo amekuwa hapatikani kwa urahisi na amekuwa na miradi mingi anayoihudumia kitu ambacho kinapelekea miradi mingine kutopata huduma kwa wakati.
Kilian Mtitu ni mtendaji kata ya Lupanga amesema kwa sasa ilitakiwa wawe wameshapiga bati lakini kutokana na mzabuni huyo bado wapo katika hatua ya kupaua huku mtendaji wa kijiji Robert Mgeni akiiomba serikali ngazi ya wilaya kuingilia kati na kumsihi mzabuni huyo kuja kumalizia ujenzi huo kwa haraka.
Kutokana na maelezo hayo ya viongozi kaimu katibu tawala huyo anaamua kumpigia simu mzabuni huyo ambapo hakuweza kupatikana kitendo ambacho kinamkasirisha na kupelekea kutoa maagizo ya kukamatwa kwake pamoja na fundi mkuu ambaye naye amekuwa haonekani mara kwa mara ili waweze kukamilisha ujenzi huo.
“Haiwezekani mtu mmoja awe kikwazo katika kuleta maendeleo, serikali imetimiza wajibu wake na wananchi nao wametimiza wajibu wao hivyo kutoleta vifaa kwa wakati ni kukwamisha juhudi za serikali”. Amesema Malamba.
Mradi huo unajengwa kwa fedha za TASAF ambapo unagharimu kiasi cha sh. Ml. 53 na unatakiwa kukamilika ifikapo juni 30 mwaka huu.