MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameonesha kwa vitendo azma yake ya kuinyanyua sekta ya kilimo na wakulima ili izidi kutoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi.
Ditopile amesema kilimo ni muunganiko wa mambo mengi ikiwemo Utafititi na Utaalamu, Kilimo ni Sayansi, Teknolojia na Mitambo, Udongo, Mbegu, Maji kwa maana ya Maji na Umwagiliaji, Dawa na miundombini ya uvunaji na uhifadhi Pamoja na Soko hivyo kuishauri Serikali kuzingatia mtiririko huo ili kuleta tija kwenye kilimo.
“Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia kwenye Nchi yetu hii ni bajeti ya kwanza inaletwa na Serikali na hakuna mtu analalamika kwamba ni ndogo hapa nimpe pongezi Rais Samia kwa hakika ameonesha yeye ni Mkulima mwenzetu na anajali kwa vitendo maslahi ya wakulima nchini na hilo amedhihirisha kwa kutuletea Waziri na Naibu Waziri wenye kujali wakulima.
Nitoe ushauri kwa Waziri na Naibu wake kuangalia watu wao wa chini haswa kwa maafisa wao ugani, Viongozi wa juu wanafanya kazi kubwa sana lakini hawa maafisa wao wa chini wanapaswa kufuatiliwa kwa karibu utendaji wao wasije kuangusha jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Samia katika kuinua Kilimo.
Unaweza kuwa na Shamba lina ekari hata 1000 lakini usione hata Afisa Ugani anakuja kukutembelea, Tumeona Rais wetu amewapa vitendea kazi ikiwemo Pikipiki, Vipimia udongo ni wakati sasa wa Serikali kuwafuatilia maafisa hawa ili wasikae tu ofisini bali waende field kutoa elimu kwa wakulima,” Mariam Ditopile.
“Niipongeze Serikali kwa kuongeza bajeti ya Kilimo hadi kufikia Sh Bilioni 751, tumeona mmehusisha vijana na niliwahi kushauri kuhusu hili kwamba vijana watengenezewe mazingira ya kushiriki kwenye kilimo na sasa tumeona kwa mipango mliyonayo kundi kubwa la vijana linakwenda kushiriki Kilimo.
Nishauri pia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara mkae pamoja mpange wote nini kinahitajika sokoni, Tuwe kama India Wizara ya Viwanda inatoa ushauri kwa Wizara ya Kilimo kwamba soko gani lipo ili wakashauri wakulima waje na zao ambalo liko sokoni hii itasaidia kukuza Soko la mazao yetu,” Mariam Ditopile.