Home Uncategorized MAADHIMISHO YA SABA YA WIKI YA UTAFITI NA UBUNIFU UDSM KUFANYIKA MEI...

MAADHIMISHO YA SABA YA WIKI YA UTAFITI NA UBUNIFU UDSM KUFANYIKA MEI 24 HADI MEI 26,2022

0

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof.William Anangiisye (katikati) akizungumza na waandishi wa habari  wakati akitoa taarifa kuhusu Wiki ya maadhimisho ya saba ya Wiki ya Utafiti  na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam yatakayoanza Mei 24 hadi Mei 26,2022 katika eneo la Maktaba mpya katika Chuo hicho.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof.William Anangiisye akizungumza na waandishi wa habari  wakati akitoa taarifa kuhusu Wiki ya maadhimisho ya saba ya Wiki ya Utafiti  na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam yatakayoanza Mei 24 hadi Mei 26,2022 katika eneo la Maktaba mpya katika Chuo hicho.

***************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WANANCHI wametakiwa kushiriki katika maadhimisho ya saba ya Wiki ya Utafiti  na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam yatakayoanza Mei 24 hadi Mei 26,2022 katika eneo la Maktaba mpya katika Chuo hicho.

Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa ambapo kauli mbiu ikiwa ni “Utafiti na Ubunifu kwa Manufaa ya Kijamii Nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 18,2022 wakati akitoa taarifa hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof.William Anangiisye amesema Chuo kitatua fursa hiyo kujipambanua katika utafiti ambao ni mojawapo ya majukumu yake makuu, kwa kuonesha shughuli zake za utafiti, huduma kwa jamii na ubadilishanaji maarifa kama njia ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii nchini.

“Kati ya miradi ya utafiti na ubunifu zaidi ya 300, mwaka huu chuo kitaonesha miradi 103 iliyofanya vyema zaidi kama vile mradi wa maabara ya kidigiali (off grid mobile universal digital laboratory) na glavu maizi kwa wenye matatizo ya kusikia na kuzungumza (smart glove for the hearing and speech impaired) pamoja na mtambo maalumu wa kuyeyusha shaba kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini”. Amesema Prof.Anangise.

Aidha Prof.Anangisye amesema wiki hii hutoa fursa ya kuimarisha ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wadau mbalimbali kitaifa na Kimataifa.Kwa kuzingati hilo, siku ya pili ya maadhimisho kutakuwa na mjadala maalum wa ushirikiano ya Kimkakati utakaowashirikisha wadau kutoka katika sekta binafsi na za umma pamoja na waandishi wa habari.

Amesema maadhimisho hayo yatatumika pia kutambua michango iliyotukuka ya wanataaluma na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam katika utafiti, ubunifu na ubadilishanaji wa maarifa.

“Katika sherehe za kufunga maadhimisho haya, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda atawatunuku tuzo watafiti na wabunifu bora katika makundi mbalimbali kama Mradi Bora wa Utafiti, Vitendo/Idara zilizoingiza kiasi Kikubwa cha Fedha za Utafiti, Vitengo/Idara zilizoingiza kiasi Kikubwa cha Fedha za Ubunifu, Watafiti walioingiza kiasi kikubwa cha Fedha za Utafiti, Mtafiti Bora, Mbunifu Bora, Miradi Bora ya Wanafunzi wa Uzamili, Miradi Bora ya Wanafunzi wa Uzamili, Miradi Bora ya Wanafunzi wa Shahada za Awali na Mradi Bora wa katika Kutoa Huduma kwa Umma”. Amesema