Mkuu wa Wilaya ya Mjini Mhe. Rashid Simai Msaraka akitoa Taarifa kwa Waandishi wa habari kuhusu Mwenendo wa Soko la Kibandamaiti kua Soko Kuu, Taarifa hiyo ametoa Ofisini kwake Amani Mjini Zanzibar.
(PICHA NA MARYAM KIDIKO – MAELEZO ZANZIBAR).
…………………………..
Na Khadija Khamis –Maelezo, Zanzibar, 19/02/2022
Mkuu wa Wilaya Mjini Rashid Simai Msaraka amesema hivi sasa minada yote inatarajiwa kufanyika katika soko la kibandamaiti na kuwa soko kuu kwa kipindi hichi hadi kukamilika kwa ujenzi unaoendelea wa masoko nchini.
Taarifa hiyo ameitoa huko Ofisini kwake Amani wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa soko la kibandamaiti kuwa soko kuu baada ya masoko yote kuwa katika harakati za ujenzi ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati.
Amesema hivi sasa halmashauri ya wilaya mjini imo katika maandalizi ya miundombinu rafiki kwa wananchi ikiwemo huduma za usafiri kwa kupanga ruti za maeneo mbali mbali na kuandaliwa kituo kikuu cha daladala.
Alieleza uwekaji wa ruti hizo na kuandaliwa kituo maalum cha daladala kwa kila njia kutasaidia wananchi kufika sokoni bila ya usumbufu wa usafiri .
Aidha amesema maeneo yameshatayarishwa kwa ajili ya kituo hicho pamoja na sehemu za magari yanayotokea shamba kwa kushusha mizigo ya bidhaa ili kuhakikisha huduma zinaendelea vizuri,
Alifahamisha katika soko hilo kutakuwa na punguzo la kila aina ya kodi ili kuhakikisha huduma zinazotolewa ziwe nafuu kuliko masoko mengine .
Nao wafanyabiashara waliopo katika soko la kibandamaiti wamesema wamefarijika kwa uwamuzi huo kwani utaweza kuwanufaisha ujio wa wateja kutokana na hivi sasa kuwa hali ya ngumu ya kibiashara.
Eneo hilo la linalotarajiwa kuwa soko kuu la kibandamaiti litakuwa la dharura ambalo litatoa fursa kwa wafanyabiashara wote kufanya kazi zao kwa muda ili kutoa huduma zitazowatosheleza wananchi.