………………………….
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ameipongeza na kuitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuendelea kuchagiza maendeleo ya Kilimo hususani Kilimo cha Mwani, Uvuvi, Unenepeshaji Kaa na Ufugaji wa Jongoo Bahari.
Amesema hayo wakati wa Kikao kazi cha Mkakati na kampeni ya kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Baharini kilichofanyika jana tarehe 24.01.2022, jijini Tanga.
Ameongeza na kusema kuwa Wananchi wanapaswa kuhakikisha wanatengeneza vyama vya ushirika ili iwe rahisi kupata mikopo kutoka TADB na kuchagiza maendeleo ya uchumi wa buluu.
Kikao hicho kilikuwa na mawasilisho mbalimbali kuhusu Dhana ya Uchumi wa Buluu, Fursa katika Ukuzaji Viumbe Maji Bahari, changamoto na mipango ya Mwaka 2022/23
TADB kupitia Afisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Biashara Bw. Furaha Sichula amewasihi wakulima na wavuvi haswa wa Mwani, Jongoo Bahari na Unenepeshaji Kaa kuhakikisha wanatengeneza Vikundi vya Ushirika ili kusaidia upatikanaji wa mikopo uwe rahisi na kuwafikia kwa wepesi.
Amewahikikishia Benki ya TADB ipo nao bega kwa bega kuhakikisha inakuza uchumi wa buluu.
Hadi sasa TADB imeidhinisha jumla ya bilioni 6.8 kwenye uvuvi kwa vyama vya Ushirika na makampuni binafsi yanayofanya shughuli za uvuvi na ufugaji wa samaki sambamba na wavuvi wadogo wadogo.