Afisa mwandamizi elimu kwa umma kutoka TMDA ,James Ndege akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha.
Afisa mwandamizi elimu kwa umma(TMDA),James Ndege akitoa maelekezo kwa mwananchi aliyetembelea katika banda hilo kupata elimu ,pembeni yake aliyesimama ni Afisa habari na elimu wa TMDA Kanda ya kaskazini ,Augustino Malamsha (Happy Lazaro)
…………………………………….
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.MAMLAKA ya dawa na vifaa tiba (TMDA) imewataka wadau wote wa maeneo ya huduma za kijamii kuhakikisha wanajenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuvutia sigara na bidhaa za tumbaku.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Afisa Mwandamizi elimu kwa umma kutoka TMDA,James Ndege wakati akizungumza katika wiki ya maadhimisho ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ambapo kilele yatafanyika kitaifa mkoani Arusha.
Ndege amesema kuwa ,hiyo ni kutokana na kanuni ya udhibiti wa tumbaku na mazao ambapo maeneo yanayotakiwa kujengewa maeneo hayo ni pamoja na vituo vya usafiri,mahoteli,nyumba za wageni,kumbi za mikutano na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ya kijamii.
“Tumetoa maelekezo kuhakikisha kuwa ndani ya mwaka mmoja wahakikishe wamejenga maeneo hayo na baada ya hapo wote watakaokikuka watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiweko kutozwa faini na kupelekwa mahakamani.”amesema Ndege.
Ameongeza kuwa,kuwepo kwa maeneo hayo maalumu yatasaidia Sana kuwaokoa na watu wengine ambao hawavuti kutopata madhara yoyote kwani moshi wa sigara una athari kubwa Sana kiafya usipodhibitiwa kwani moja ya jukumu la mamlaka hiyo ni kulinda afya ya walaji kwa kudhibiti uvutaji holela.
Aidha amesema kuwa, katika kuhakikisha wanadhibiti uvutaji huo kwa watoto chini ya miaka 18 wameelekeza viwanda vyote vinavyotengeneza kuhakikisha wanaweka tangazo la kuwa “ni marufuku kwa watoto chini ya miaka 18 kuvuta sigara hiyo ili kuokoa vijana hao kwani vijana wengi wanaharibika kutokana na uvutaji huo.”amesema.
Aidha amewataka wavutaji wa sigara kutokuvuta maeneo ya wazi ili isiwaathiri watu wengine ambao hawavuti kwani moshi wa sigara unasababisha damu ambayo inasambazwa mwilini huchafuliwa na kemikali zenye sumu ambapo kemikali hizo zinaweza kuharibu moyo na mishipa ya damu,ambayo inaweza kusababisha magonjwa ya moyo.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuwa na tabia ya kwenda kupima afya zao mara kwa Mara badala ya kutumia dawa kiholela pindi wanapojisikia vibaya bila kupima na kutaka kujua wana matatizo gani ,hivyo kuwataka kupima afya zao mara kwa mara ili waweze kupata tiba mapema.
“Wananchi wengi wana changamoto kubwa sana ya kuchukua dozi na kutumia nusu wengi wao hawamalizi dozi, hali ambayo inachangia wale wadudu kurudi tena ,hivyo amewataka kutumia dozi yote kama walivyopewa na kutokatiza dozi hiyo.”amesema Ndege.