Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi akizungumza katika mkutano wa Mawaziri wa Kisekta kutoa mrejesho maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji mkoa wa Tabora.
Sehemu ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakiwa katika mkutano wa wananchi katika kijiji cha Kigwa wilayani Uyui mkoa wa Tabora. Wa nnne kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt Batilda Burian
……………………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
SERIKALI imesema kwamba wakazi wa vijiji 94 kati ya 100 vya Mkoa wa Tabora ambavyo vilikuwa na migogoro ya ardhi kuendelea kuishi katika maeneo hayo wakati utaratibu mwingine wa kuweka mipaka ukiendelea.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatilia na kutatua migogoro ya ardhi katika mikoa yote, William Lukuvi wakati akiwasilisha Taarifa juu ya maamuzi waliyofikia juu ya Vijiji 100 vya Mkoa wa Tabora.
Waziri Lukuvi aliwaelekeza Watendaji wote wa ngazi ta Mkoa na Wilaya kusimamia zoezi la uwekaji wa mipaka mipya ya maeneo yaliyokuwa na migogoro bila ya kuleta taharuki kwa wananchi wa maeneo husika.
Aliongeza kuwa zoezi la kuanisha mipaka litafanyika ili wananchi wasiendelee kuvamia maeneo ya hifadhi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya sasa na kizazi kijacho.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kaliua Alyoce Kwezi aliishukuru kwa kurasimisha baadhi ya vijiji vya Kaliua ambavyo vilikuwa katika migogoro wa ardhi na kuiomba Serikali kutatua mgogoro uliozuka baada ya Hifadhi ya Msitu wa ISAWIMA kupandishwa hadhi.
Alisema baada ya Serikali kukabidhi usimamizi wa ISAWIMA kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) kumekuwepo na mgogoro mkubwa na vijiji 11 ambavyo ndivyo vilitoa ardhi yao kwa ajili ya uanzishwaji wa ISAWIMA.
Kwezi alisema TAWA wameongeza mipaka na kuingia katika maeneo ya wananchi jambo ambalo limesababisha taharuki kubwa ya wakazi kukosa mashamba ya kulima wakati masika.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Kamati hiyo Lukuvi aliutaka uongozi wa Mkoa wa Tabora kutumia wataalamu waliopo kushughulikia mgogoro wa mpaka baina ya Wilaya ya Kaliua na Urambo.
Alisema tangazo lililoanzisha wilaya hizo lipo ni vema wakarejea kwenye kumbukumbu hizo na kuondoa dosari ambazo zimesababisha mgogoro wa mpaka katika maeneo hayo.
Lukuvi alisema baada ya usuluhisho huo ni vema Serikali ya Mkoa ikaiandikia Tume ya Uchaguzi ya Tanzania(NEC) itumie ramani iliyosainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio walionayo kwa kuwa inasababisha mgogoro.