Moshi, Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Profesa Patrick Ndakidemi amewaasa wananchi kuendelea kula vyakula vya asili kwani vinafaida kubwa mwilini ikiwamo kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Prof. Ndakidemi ametoa kauli hiyo leo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya chakula duniani ambapo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Mandela Pasua manispaa ya Moshi.
Amesema kuwa, maonyesho hayo ya siku ya chakula yanawakumbusha mengi wananchi katika kulinda afya zao ikiwamo ulaji wa vyakula vya asili.
“Tukiendelea kuzingatia ulaji wa vyakula vya asili afya zetu zitaendelea kuboreka na maisha yetu yatakuwa mazuri pia tutajikinga na magonjwa mbalimbali” amesema Ndakidemi.
Ameongeza kuwa, vyakula vya asili vimekuwa vikipatika katika maeneo wanayoishi wananchi na kwa gharama nafuu.
Aidha Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kutumia maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni Oktoba 17 mwaka huu kutembelea mabanda mbalimbali yaliyopo uwanjani hapo kupata elimu juu ya mlo bora hasa vyakula vya asili.
Prof. Ndakidemi alisema kuwa, vijana wamekuwa wakiishia kula chipsi na kuku za kisasa na kuvisahau vyakula vya asili ambavyo husaidia mwili kujikinga na magonjwa.