WANACHAMA na Wastaafu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wamesogezewa huduma za Mfuko kwa kutumia simu ya
kiganjani na wanachotakiwa kufanya ni kujiunga na Mfumo wa PSSSF Kiganjani na PSSSF Popote
Mtandao, Meneja wa Mfuko huo
Mkoani Geita Bw. Geofrey Kolongo amewaambia waandishi wa habari.
Akizungumza kwenye banda la PSSSF kwenye Maonesho ya
Nne ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayofanyika kwenye
viwanja vya EPZA eneo la Bombambili Mkoani Geita Septemba 23, 2021, Bw. Kolongo
alisema Mfumo huo sio tu unarahisisha upatikanaji wa huduma lakini pia unaokoa muda na kupunguza gharama.
“ Mwanachama akijiunga na mfumo huu halazimiki
kutembelea ofisi zetu kupata huduma, badala yake atapata huduma za Mfuko akiwa
kwenye shughuli zake au nyumbani,” alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu Mfumo huo, Bw. Kolongo
alisema ili kutumia Mfumo wa PSSSF Kiganjani Mwanachama atajisajili ili kupata
akaunti ya mtumiaji, kisha ataweza kuona michango na taarifa zake za msingi za
mwanachama na kwa Mstaafu ataweza kuona taarifa zake za msingi ikiwa ni pamoja
na kuona kumbukumbu za malipo ya pensheni ya kila mwezi.
Kuhusu PSSSF Ulipo Mtandao, Bw. Kolongo alisema Mfumo
huo unajumuisha Madirisha (Portals) Matatu moja la Mwanachama (Member Portal)
linalomuwezesha kuangalia taarifa zake za msingi za uanachama kuangalia Taarifa
zake za Michango na kuwasilisha Maulizo mbalimbali kuhusiana na Michango au Uanachama
na lolote linalohusiana na Mfuko.
Akieleza zidi Meneja huyo alitaja Dirisha la Pili ni
la Muajiri (Employer Portal) ambaye anaweza kuangalia taarifa zake za michango,
kuangalia taarifa za madai yahusuyo Taasisi yake yaliyowasilishwa, na anaweza
kuwasilisha maulizo ya aina yoyote na Dirisha la Tatu ni dirisha la Malipo
(Billing System/Portal) Mfumo huu hutumika kwa ajili ya ukusanyaji wa michango
na umeunganishwa na mifumo ya ndani na ule wa malipo ya Serikali, Mfumo utamuwezesha
mwajiri kupata control namba inayotumika kwa malipo ya Serikali na anaweza
kupata risiti na kuiprinti.
Maonesho hayo yanayoandaliwa kila mwaka na uongozi
wa Mkoa wa Geita yalianza Septemba 16 na kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa Septemba 22, 2021 na yamebeba kauli mbiu isemayo “ Sekta ya Madini kwa Ukuaji wa Uchumi na
Maendeleo ya Watu.”