Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo (kulia) wakati akiagana nae baada ya kumaliza kikao chao kilichofanyika jijini Dodoma Julai 27, 2021. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiwa katika picha mara baada ya kumaliza kikao chao kilichofanyika jijini Dodoma Julai 27, 2021. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.
………………………………………………………..
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipatia Kampuni ya Chobo Kitalu mbadala katika eneo la Mradi wa Mwisa II lililopo Wilayani Muleba, Mkoani Kagera baada ya kuchelewa kuendeleza Kitalu cha awali ilichopewa katika Ranchi ya Mabale iliyopo Mkoani humo na kupelekea wawekezaji wengine kutumia eneo hilo.Ndaki alitoa agizo hilo katika kikao chake kilichoshirikisha Mwekezaji huyo, Viongozi wa NARCO na wadau wengine kilichofanyika jijini Dodoma Julai 27, 2021.
Kufuatia maamuzi hayo, Waziri Ndaki ameielekeza NARCO kushughulikia jambo hilo kwa haraka ili mwekezaji huyo aweze kuendelea na shughuli zake za uwekezaji nchini.
“Kama nilivyosema sisi tuko tayari kushirikiana na Chobo pamoja na wawekezaji wengine kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya mifugo ili kutimiza malengo ya Tanzania ya Viwanda,” alisema Ndaki
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo pamoja na kumshukuru Waziri kwa hatua hiyo, alisema kuwa uamuzi huo utasaidia kiwanda chake kupata malighafi iliyobora kutoka kwa mifugo watakayoiwekeza katika eneo hilo na anaamini kwa ushirikiano wanaopata kutoka kwa NARCO na Wizara wataweza kuzalisha bidhaa bora itakayoweza kushindana katika Soko la Kimataifa.
Aliongeza kuwa kiwanda chake cha kuchakata nyama ni kikubwa na kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 600 na mbuzi 1500 kwa masaa nane, hivyo kupitia uwekezaji huo kampuni yake itaweza kutengeneza mnyororo wa thamani utakaoweza kufaidisha maelfu ya Watanzania.
Julai 9, 2021 Waziri Ndaki alipokuwa katika ziara Mkoani Kagera alimtaka mwekezaji huyo kukubali kuachia Kitalu cha Mabale ili kuepusha mgogoro uliopo baina yake na wawekezaji wengine ambao wanatumia eneo hilo alilokabidhiwa awali na kumuahidi kuwa pindi atakapokuwa tayari kuwekeza Wizara itampatia eneo mbadala ambalo litakuwa zuri zaidi kwa uwekezaji wake.