………………………………………………………………………….
NA MWANDISHI WETU
Watoa huduma za simu nchini wamepongeza uamuzi wa hivi karibuni wa serikali katika kuangalia upya kodi za miamala ya simu iliyotokana na sheria mpya ya fedha kwa mwaka 2021/22, huku wakisisitiza kuwa uamuzi huo utaongeza chachu katika uwekezaji ndani ya sekita hiyo.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na mwenyekiti wa chama cha waendesha huduma ya simu za mkononi Tanzania (TAMNOA), Hisham Hendi, ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom.
Alisema kuwa wateja zaidi ya milioni moja hususani walioko vijijini walisitisha kutumia huduma za miamala ya simu kutokana na ongezeko la makato ambayo alisema yalitishia uhai wa biashara ya simu nchini.
“Katika siku chache zilizopita tangu sheria ya fedhja ilipoanza kutekelezwa julai 15, miamala ya wateja ilipungua kwa asilimia 45, jambo ambalo limeathiri mapato ya kampuni za simu na hivyo kupunguza kodi kwa serikali,’’ alisema na kuongeza:
“Tunaishukuru serikali kwa kuona umuhimu na binafsi tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kusikiliza kilio cha wananchi.’’
Waziri mkuu Kassim Majaliwa alifanya kikao na mawaziri pamoja na wadau wa sekta ya mawasiliano kutatua changamoto hiyo ambapo kikao hicho kilikuja na mapendekezo ya kutatua changamoto iliyo jitokeza.
Timu iliyoundwa na Waziri mkuu hivi karibuni itakaa na kampuni za simu na benki kuu ili kuangalia mambo yote yanayohusu kodi ili kuyatafutia ufumbuzi.
Kulingana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba, timu hiyo inajumuisha wataalamu kutoka Benki Kuu, Mamlaka ya Mwasailiano Tanzania (TCRA),Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Hata hivyo bwana Hendi alisisitiza kuwa ana imani na matokeo na mapendekezo ambayo yatatolewa na timu hiyo iliyoundwa na waziri mkuu huku akisisitiza kuwa kampuni za simu zitakuwa na uwezo mkubwa kibiashara hapa nchini.
Aliongeza kuwa Tanzania hivi sasa inajivunia ukuaji wa uchumi barani Afrika kutokana na uwekezaji mkubwa wa kampuni za simu.
Kulingana na takwimu za masuala ya mawasiliano zilizotolewa hivi karibuni na taasisi ya masuala ya mawasiliano ya GSMA, kunapokuwa na huduma nafuu za mawasiliano popote duniani, kuna uwezekano mkubwa wa kuboresha seka mbalimbali hasa ya kilimo na afya.
Hivi karibuni, bunge lilipitisha sheria ambayo ilitoa tozo ya kodi ya miamala ya simu ambayo imesababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa mawasiliano, jambo ambalo lilimfanya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuunda timu ya wataalamu kushughulikia suala hilo.
Juma lililopita Waziri wa Fedha na Mipango, Dr Mwigulu Mpango aliueleza umma kwamba Rais Samia amesikiliza kilio cha wananchi na kutoa maelekezo ya namna ya kushughulikia suala hilo.
MWISHO