Mbunge wa Ukonga Jerry Silaa amesema imefikia hatua Wabunge waanze kulipa kodi kupitia mishahara yao ili wapate uwezo wa kuwaambia Wananchi na wao walipe kodi.
Silaa ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliowashirikisha wananchi wa Mzinga Ukonga jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo jimboni kwake.
“Mie nimeanza Ubunge juzi mwaka jana mwezi wa 11, kwahiyo nimekuta hayo yanayosemwa mengine yameshapitishwa tayari Bungeni na katika hili niungane na Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba kwamba vikiliwa vya Mwali na vya Kungwi viliwe”
“Ni wakati muafaka sisi Waheshimiwa Wabunge ili tupate uwezo wa kuwaambia Watu waanze kulipa kodi na sisi tuanze kulipa kodi katika mishahara yetu, hakuna sababu ya kuwa wengine wanalipa wengine hawalipi ukishakuwa haulipi unakosa ile nguvu ya kumwambia mwenzako alipe”
“Kwahiyo niseme tu kwamba kazi kubwa inayotakiwa tuifanye sisi kama viongozi ni kutowadanganya Watanzania kwamba tunaweza kuiendesha nchi bila Kodi, haitowezekana”