…………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
Benki ya Mwalimu (Mwalimu Commercial Bank Plc) inajivunia kutimiza miaka mitano ya mafanikio tangu kuanzia kwake Julai 22, 2016 na kuanza kutoa huduma bora kwa Wateja wake na Jamii kwa ujumla wakiwemo Walimu, Wawekezaji na Wafanyakazi katika Sekta na Taasisi mbalimbali nchini.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Benki hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa MCB, Richard Makungwa amesema wanajivunia miaka mitano ya mafanikio kutoa huduma bora kwa jamii ya Watanzania hadi kufikia mwaka huu wa 2021 ikiwa pamoja na malengo ya kuboresha mnyororo wa thamani wa Elimu ifikapo 2025 kupitia mkakati wake kupitia ikolojia ya elimu.
Makungwa amesema hadi sasa wanajivunia kuwa na Wateja zaidi ya elfu Arobaini sambamba na kuwa na amana ya kiasi cha pesa Shilingi Bilioni 27 zilizosaidia kukopesha Wateja wa Benki hiyo, amesema tangu kuanzishwa kwake wanajivunia kutoa mikopo jumla ya kiasi cha pesa Shilingi Bilioni 60 huku wanufaika wakubwa wakiwa Walimu katika kipindi chote cha miaka mitano ya utoaji huduma.
Amesema kuna idadi ya Walimu takriban Laki Mbili na Kumi na Saba (217,000) ambao ni Wawekezaji wakiwa na asilimia 35 (35%) sambamba na sehemu ya Umma wa Watanzania wenye asilimia 16 (16%) pekee, amesema Benki hiyo imefanya maboresho hadi sasa kuwa na Mtandao wa Simu za Mkononi (Mobile Banking) unaojulikana kama Mwalimu Mobile ambao unawasaidia kufanya miamala mbalimbali kupitia Simu.
“Mwaka huu (2021) wa mafanikio tumeingia kwenye Mfumo wa VISA ambapo sasa unasaidia kufikia Wateja wengi zaidi kufanya miamala na kupata huduma zetu kupitia ATM yoyote nchini Tanzania, pia tuna Mawakala (Mwalimu Wakala) zaidi ya 200 Tanzania nzima”, amesema Makungwa.
Benki ya Mwalimu imesajiliwa katika Soko la Mitaji, Wamiliki wakubwa wakiwa Chama cha Walimu Tanzania, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) wakati hadi sasa ikiwa na Ofisi zake mkoani Dar es Salaam, Mlimani Tower ambapo ni Makao Makuu, Mtaa wa Samora, Posta sambamba na Ofisi tano zilizopo, Arusha, Morogoro,Dodoma, Mwanza na Mbeya.