Home Mchanganyiko  HUDUMA YA AFYA/ ELIMU ZAWATESA WANANCHI LUDEWA, WANAFUNZI WATEMBEA KM. 8 KUFUATA...

 HUDUMA YA AFYA/ ELIMU ZAWATESA WANANCHI LUDEWA, WANAFUNZI WATEMBEA KM. 8 KUFUATA ELIMU.

0

………………………………………………………………………..

Na. Damian Kunambi, Njombe.

Wakazi wa kitongoji cha Luhuhu getini kilichopo katika kata ya Mavanga wilayani Ludewa mkoani Njombe wameiomba serikali kuwapa kijiji ili waweze kupata huduma za msingi kama shule na kituo cha afya kwani kwa sasa huduma hizo wanazifuata umbali mrefu.

Wakizungumza hayo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipofanya ziara katika kitongoji hicho, wakazi hao wamedai kuwa watoto wao wanatembea umbali wa kilometa 8 kufuata elimu kitu ambacho kinawakatisha tamaa watoto hao ya kuendelea na masomo huku zahanati ikiwa mbali kiasi cha kushindwa kufikika kwa kutembea.

Michael Mgaya ni mmoja wa wakazi hao amesema kuwa umbali wa huduma hizo imekuwa ni kero kwao hasa wanafunzi ambapo wanalazimika kutoka majumbani usiku sana ili wawahi shuleni na inapofika kipindi cha mvua wanafunzi hao hulazimika kutokwenda shule maana njia wanayotumia kuna mto ambao hujaa maji na kuwafanya washindwe kuvuka.

Naye Martina Mkinga ni mkazi wa kitongoji hicho na mjumbe wa shule ya msingi Ushindi amesema amekuwa akiwakusanya wanafunzi hao saa tisa hadi kumi usiku kwa kugonga kengele iliyofungwa katika kitongoji hicho na wakisha kusanyika huanza safari ya kuwapeka shuleni kwa pamoja.

” Ili kuwasaidia wanafunzi hawa waweze kufika shuleni mapema na kuwahi masomo yao, kila siku nimekuwa nikiwakusanya na wakupeleka shuleni kwakuwa muda wanaotoka nyumbani huwa ni usiku sana hivyo ni vigumu kutembea peke yao”, Alisema Martina.

Angel Luoga ni mwanafunzi wa shule hiyo amesema umbali wa shule unawapa shida sana kwakuwa wamekuwa wakichelewa masomo na wakifika shuleni husinzia kutokana na kuamka usiku na kutembea umbali mrefu kitu ambacho hupelekea kutofanya vizuri katika masomo yao hivyo wanaiomba serikali kuwasaidia kupata shule jirani.

Kwa upande wa diwani wa kata hiyo Daud Luoga amesema kuwa tayari wanakitongoji hao wameanza kuandaa mazingira ya kuweka kijiji kwani wameshaanza kujenga darasa moja katika eneo walilopendekeza kuweka shule na lina ukubwa wa hekari nane sambamba na kutenga eneo la kituo cha afya.

Amesema kitongoji hicho kina wakazi 420 hivyo wamekubaliana kuungana vitongoji vitatu ili kuwa kijiji ambavyo ni kitongoji cha Mgombezi, Ushindi na Luhuhu getini ambapo vijiji hivyo vikiungana vinaweza kufanya maendeleo na kupata huduma kwa ukaribu zaidi.

Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amekubaliana na hoja hiyo ya kuanzisha kijiji na kumtaka mwenyekiti wa kijiji kumkabidhi mihutasari yote ili aweze kuiwasilisha TAMISEMI na kuanza mchakato wa kupata kijiji hicho.

Amesema kwakuwa tayari wameanza mchakato wa ujenzi wa taasisi mbalimbali ambazo ni muhimu na ni moja ya sifa ya kupata kijiji hivyo waendelee na ujenzi wa shule hiyo pamoja na zahanati na yeye ataenda kushughulikia suala hilo la kupata kijiji.

Ameongeza kwa kuwaomba wananchi kuendelea kujitoa kutumia nguvu zao katika ujenzi wa shule hiyo ambayo tayari wamekamilisha kwa kuezeka chumba kimoja ili waweze kuifikisha katika hatua ambayo serikali itawasaidia kuimalizia.

” Mimi niko pamoja na nyie katika kila hatua, naomba mpange siku ili nije tusaidiane katika kufyatua tofali nami nataka nichangie nguvu zangu katika ujenzi huu ili watoto wetu waondokane na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu”, Alisema Kamonga.