Afisa Kilimo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw.Azizi Mtambo (mwenye shati jeupe)akitoa zawadi kwa mdau aliyetembelea banda la Mamlaka jana tarehe 2.7.2021.
********************
Wazalishaji wa mbolea nchini watakiwa kuongeza uzalishaji ili kuweza kukuza soko la mbolea ndani na nje ya nchi na kuwezesha nchi kuwa kitovu cha biashara hiyo kwa nchi ambazo zinaizunguka.
Ameyasema hayo jana, Kaimu Meneja Uingizaji na Usafirishaji wa Mbolea Nje ya Nchi.(TFRA), Bw.Mselem Seleman katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba),yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Aidha Bw.Seleman amesema kwa mwaka huu Tanzania inazaidi ya tani laki 1.5 za mbolea ambazo tayari zimeshatolewa kibali kusafirishwa kwenda nje ya nchi hivyo kuna umuhimu wa wafanyabiashara kuongeza uzalishaji wa mbolea kuweza kuongeza soko hilo.
“Nchi ambazo zimetuzunguka zinatumia sana mbolea kupitia hapa Tanzania, moja wapo ya nchi hizo ni Rwanda, Burundi,Congo,Zambia, Malawi na nyingine Kenya”. Amesema Bw.Seleman.
Sambamba na hayo Bw.Seleman amesema kuwa mfanyabiashara ambaye atatakiwa kusafirisha mbolea nje ya nchi anapaswa kuomba kibali kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kupitia mtandao.
Kwa upande wake Afisa Ubora wa Mbolea (TFRA), Bw.Raymond Konga amesema kila mbolea au kisaidizi cha mbolea lazima isajiliwe na Mamlaka hiyo kabla haijaanza kutumika nchini kwa mujibu wa kifungu namba 8 cha sheria ya mbolea.
Pamoja na hayo amesema hairuhusiwi kwa mtu yeyote kuingiza mbolea nchini isipokuwa awe amepata kibali kutoka katika mamlaka kwa mujibu wa kifungu na.21.
“Uingizaji wa mbolea nchini unafanyika kwa njia mbili ambapo ya kwanza ni kwa kutumia mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja.Mfumo huu unasimamiwa na kanuni za ununuzi wa mbolea kwa pamoja, njia ya pili ni uingizaji wa mbolea kwa mfumo huria.Katika mfumo huu kila mtu anaruhusiwa kuingiza mbolea ilimradi amefuata sheria na taratibu za uingizaji wa mbolea”. Amesema Bw.konga.
Sanjari na hayo TFRA inawakaribisha wadau na wananchi kwa ujumla kutembelea banda lao katika maonesho ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Sabasaba Jijini Dar es Salaam.