Mhitimu wa mafunzo ya kozi maalum namba 17/2021 ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu Idd Namanolo akimuonesha Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Alkwin Ndimbo aliyevaa Suti, vitambaa vilivyowekwa mafuta machafu ambayo yanasaidia kufukuza Tembo kabla ya kuingia kwenye mashamba na makazi ya watu wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo katika chuo cha Uhifadhi wa maliasili kwa jamii Likuyu Sekamaganga wilaya ya Namtumbo,kushoto kwake mkuu wa chuo hicho Jane Nyau.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya kozi maalum namba 17/2021 ya askari wanyamapori wa vijiji(VGS) katika chuo cha mafunzo ya Uhifadhi wa maliasili kwa jamii Likuyu Sekamaganga,wakionesha namna ya kutoa msaada kwa askari aliyejeruhiwa na wanyama wakali wakati wa operesheni kwenye hifadhi wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo jana.
Mmoja wa askari wanyamapori aliyehitimu mafunzo ya kozi maalum namba 17/2021 katika chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi Maliasili kwa Jamii(CBCTC)Likuyu Sekamaganga wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambaye hakufahamika jina lake,akionesha umahiri wa kuruka viunzi akiwa porini wakati wa mahafali ya kuhitimisha mafunzo hayo jana.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya kozi maalum namba 17/2021 ya askari wanyamapori wa vijiji(VGS)katika chuo cha Mafunzo ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii(CBCTC)Likuyu Sekamaganga wilayani Namtumbo, wakimsikiliza jana mwakilishi wa Mkuu wa wilaya hiyo Alkwin Ndimbo(hayupo pichani) wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa askari 106 wa wanyamapori wa vijiji.
Picha zote na Muhidin Amri
………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Ruvuma
JUMLA ya askari 106 kati 110 wa wanyamapori wa vijiji(VGS)kutoka jumuiya za wanyamapori nchini, wamehitimu mafunzo ya kozi maalum katika chuo cha mafunzo ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii Likuyu Sekamaganga wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mkuu wa chuo hicho Jane Nyau amesema,mafunzo hayo ni mkakati wa Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu askari hao wa vijiji kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa jamii zinazoishi kando kando ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Nyau alitaja jumuiya wanazotoka wanafunzi hao hao ni hifadhi ya msitu wa Engoserosambu wilaya ya Ngorongoro ni 6 , na 100 wanatoka jumuiya za Mbarang’andu,Kimbanda na Kisungule zilizopo wilaya ya Namtumbo na jumuiya ya Nalika na Chingolo iliyopo katika wilaya ya Tunduru kwa ufadhili wa Shirika la Word Wide Fund For Nature(WWF).
Hata hivyo amesema, wanafunzi wanne waligomea mafunzo na kuondoka chuoni ambao ni Jafari Abdala,Mohamed Mchamedi wa jumuiya ya Chingoli,Swalehe Mbalale wa jumuiya ya Nalika na Milkion Ponera wa jumuiya ya Kimbanda.
Amesema, chuo hicho ni mojawapo ya vyuo vya Serikali chini ya Wizara ya maliasili na utali chenye wajibu wa kutekeleza mkakati huo kwa kuijengea jamii uwezo kwa njia ya mafunzo ili iweze kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa lengo la kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Mkuu huyo wa chuo amesema, ni ukweli usiopingika kuwa,kwa sasa idadi ya watu nchini imeongezeka na ongezeko hilo linakwenda sambamba na shughuli za kibinadamu kama kilimo,ufugaji na nyinginezo hali inayopelekea mwingiliano kati ya shughuli za binadamu na rasilimali za maliasili.
Alibainisha kuwa, kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kumepelekea kukithiri kwa uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti,kuziba kwa shoroba, maeneo mtawanyiko wa wanyamapori,uharibifu wa vyanzo vya maji na athari nyingine.
Amesema, matumaini ya serikali chini ya wizara ya maliasili na utalii wahitimu hao watakuwa mabalozi na walimu wazuri kwa jamii na kupeleka elimu hiyo kwa wananchi wa maeneo yao ili nao waweze kunufaika.
Aidha,amewashauri wananchi hasa wanaoishi kando kando ya maeneo ya hifadhi, kuanza kulima mazao ambayo hayapendwi kuliwa na wanyamapori kama Tembo,ikiwemo ufuta,alizeti na kupanda pilipili kuzunguka mashamba yao kama njia mbadala ya kuepuka kuvamiwa na wanyama hao katika maeneo yao.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Alkwin Ndimbo amewaasa wahitimu hao kutambua kwamba, kazi ya uhifadhi inahitaji uzalendo,uadilifu na uaminifu katika ulinzi wa rasilimali za nchi yetu.
Hivyo amewataka kwenda kusimamia vyema tunu na rasilimali za nchi, na kujiepush na tamaa wakati wote wa majukumu yao ya ulinzi ili kuleta tija kwa jamii na nchi kwa jumla.
Amesisitiza, suala la uzalendo na uvumilifu kwani ndiyo sehemu wajibu katika kazi za kila siku na ni sehemu ya kiapo chao tofauti na watumishi wengine wa umma.
Amewaasa kwenda kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria za uhifadhi na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu kwa jamii inayowazunguka badala ya kutumia mafunzo waliyopata kunyanyasa wananchi wengine hasa pale zinapofanyika operesheni za kuwaondoa wavamizi kwenye misitu na rasilimali mbalimbali.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu Masoud Nyoni amesema, katika mafunzo hayo wamepata elimu stahiki juu ya uhifadhi na matumizi ya endelevu ya maliasili vijijini kwa maendeleo endelevu.
Amesema,elimu hiyo imegusa nyanja mbalimbali za uhifadhi wa maliasili kupitia masomo tofauti kama sheria za uhifadhi,utambuzi wa wanyamapori na matumizi ya silaha hifadhini.
Kwa mujibu wa Nyoni,mafunzo mengine ni matumizi ya GPS na ramani,huduma ya kwanza,maadili katika uhifadhi,ukakamavu,haki za binadamu,mbinu za doria,intelejensia,upelelezi,upekuzi na ukamataji majangili.
Ameiomba Serikali kuboresha mazingira ya mafunzo kwa wanafunzi wa chuo kama upungufu wa mabweni,vitendea kazi kama silaha,fedha,mahema,GPS,radio call, na viona mbali.